UCHAGUZI WA BODI YA LIGI KUFANYIKA IJUMAA@GOLDEN JUBILEE TOWER

Uchaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) utafanyika Oktoba 25 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL). 
Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.
 
RAMBIRAMBI MSIBA WA JIMMY MHANGO
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wa Bodi ya klabu ya Ashanti United, Jimmy Mhango kilichotokea jana (Oktoba 21 mwaka huu). 
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mhango aliutumikia mpira wa miguu kwa muda mrefu, tangu akiwa mchezaji, kocha na baadaye kiongozi. 
Kabla ya kuingia kwenye Bodi ya Ashanti United, enzi za uchezaji wake alichezea timu za Mapinduzi ya Dodoma, Ushirika ya Moshi na Pan African ya Dar es Salaam. Pia aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Ashanti United.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mhango, klabu ya Ashanti United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Maziko yamefanyika jana mchana katika makaburi ya Abeid (Mchikichini) Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Mhango mahali pema peponi. Amina

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)