IMANI MADEGA:ALIVYOPANIA KUPELEKA MBELE SOKA LA TANZANIA IWAPO ATACHAGULIWA MAKAMU WA RAIS TFF

IMANI OMARI MADEGA

Na Deodatus Mkuchu, gazeti la Tanzania Daima
UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), umepangwa kufanyika Oktoba 27, ukitanguliwa na ule wa Bodi ya Ligi Kuu ambao utafanyika siku mbili kabla; yaani Oktoba 25.
Ni uchaguzi utakaohitimisha utawala wa Rais Leodegar Chilla Tenga aliyeingia madarakani mara ya kwanza Desemba 27, 2004 kabla ya kutetea kiti hicho uchaguzi uliofuata wa Desemba 14, 2008.
Miongoni mwa wagombea wa nafasi ya Makamu wa Rais, ni Imani Mahugila Madega, atakayechuana na Ramadhan Nassib aliyewahi kuwa Makamu wa Pili wa Shirikisho hilo akiwakilisha Klabu za Ligi Kuu na Wallace Karia, Mwenyekiti wa Kamati Mpito ya Ligi.
Katika mahojiano yake na Tanzania Daima, Madega anasema amejitosa kwenye nafasi hiyo ili kutumia elimu, vipaji alivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu na uzoefu kusaidia harakati za kuendeleza mchezo huo.
Madega, mwanasheria kitaaluma, anasema kwa vile amekuwa na uzoefu wa kutosha wa kuongoza soka kuanzia ngazi ya klabu, mkoa hadi taifa, haendi TFF kujaribu kuongoza bali akiwa na uhakika wa nini anakwenda kufanya.
“Nina kiu ya kuleta mageuzi zaidi ya soka kwani kwa kipindi cha zaidi ya miaka nane ambayo nimekuwa kwenye uongozi kuanzia ngazi ya klabu, mkoa hadi taifa, nimejifunza mengi, hivyo nagombea nikijua nakwenda kufanya nini kama nitachaguliwa,” anasema.
Madega anasema akiwa mwenyekiti wa Yanga (2007-2010), alijifunza mengi hivyo anajua klabu zinahitaji nini ziweze kupiga hatua zaidi kisoka na kiuchumi kwa maslahi ya vijana.
Anasema kwa vile michezo sasa si afya na burudani tu kama ilivyokuwa zamani hasa kutokana na kuwa ajira kwa wenye vipaji na taaluma mbalimbali, kumbe ni sekta inayohiji uwekezaji wa nguvu.
Madega anasema kwa miaka minne aliyokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF 2004 -2008 na baadaye kuwa mjumbe wa Kamati ya Maadili na Hadhi za Wachezaji kwa miaka minne 2008 hadi 2013, anayajua mengi.
“Naamini kupitia taaluma yangu ya sheria, uzoefu wangu wa kuongoza kuanzia ngazi ya klabu, mkoa hadi taifa na kukulia mazingira ya soka tangu nikiwa shuleni, najua vitakuwa chachu ya mafanikio,” anasema.
Anaongeza, kwa vyote hivyo alivyojaaliwa kuwa navyo, anajiona mwenye deni kwa taifa lake, hivyo namna pekee ya kulipa ni kuitumikia soka akiwa Makamu wa Rais wa TFF.
Anasema pamoja na kutambua weledi wa wajumbe wa mkutano mkuu katika kufanya maamuzi kwa maslahi ya soka la Tanzania, bado anawakumbusha kuwa wasifanye makosa ambayo yataligharimu soka kwa miaka minne.
“Nawasihi na kuwaomba wajumbe wa Mkutano Mkuu kwamba wana deni kubwa kwa Watanzania, hivyo wanapaswa kufanya maamuzi yatakayoleta mageuzi ya mchezo huo kwa kuchagua viongozi wenye uwezo na waadilifu.”
Anasema hatakuwa sahihi akisema uongozi wa Rais Leodegar Chilla Tenga haujafanya kitu kwa sababu umefanya mengi hasa kujenga misingi imara ya utawala wa mchezo huo kiasi kwamba imekuwa taasisi kamili.
Madega anasema pamoja na mafanikio hayo chini ya mgawanyo wa majukumu kupitia idara mbalimbali, pia yapo mengi yanayohitaji kufanyiwa kazi zaidi na viongozi wajao.
Anasema msingi bora uliojengwa chini ya utawala wa Tenga, umeifanya TFF kuaminika mbele ya wadau na jamii na kusema kama atashinda, kazi mojawapo ni kuyaenzi kisha kupiga hatua mbele zaidi hasa uwekezaji.
Madega anasema uwekezaji ambao kama atashinda ataupigania zaidi ni soka ya vijana akiamini ndio msingi wa mafanikio ya mchezo huo duniani kote.
Jambo jingine ambalo atalisimamia ni soka ya wanawake ambayo licha ya uwepo wa vipaji vingi kila kona nchini, hakuna ligi wala mashindano ambayo vijana wataonyesha uwezo wao ili kutwaliwa na timu mbalimbali.
Uwazi
Madega anasema chini ya Tenga, TFF imejitahidi kujenga uaminifu mbele ya jamii na ndio maana leo hii soka imekuwa na wadhamini mbalimbali kama Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Kilimanjaro Premium Lager na Coca Cola inayodhamini michuano ya vijana wa chini ya miaka 15.
Aidha, kuna wadhamini wa Ligi Kuu, kampuni ya Vodacom na wengineo wadogo kama Uhai kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vijana wa chini ya miaka 20, lakini bado juhudi zinatakiwa za kuwapata wadhamini zaidi katika mchezo huo.
“Kazi ya TFF si kuuza soda, bali kuendeleza soka, hivyo pamoja na juhudi kubwa iliyofanywa na Tenga, soka haijawa na heshima yake kwa asilimia 100 kwa sababu yapo makosa yalifanyika,” anasema.
Madega anasema, baada ya Tenga kujenga msingi, kazi iliyobaki ni soka kuchezwa kwa maana ya kuwa na mfumo bora zaidi wa ligi kuwezesha mchezo huo kuchezwa mikoa yote.
Anasema kitendo cha soka kuonekana kuchezwa au kunawiri kwa baadhi tu ya mikoa, si kitu kizuri kama kweli tunataka mchezo huo ufike kwenye mafanikio makubwa kwa maslahi ya vijana na taifa kwa ujumla.
Soka ya vijana/ wanawake
Madega anasema kwa kutambua nini msingi wa mafanikio ya soka kote ulimwenguni, kama atachaguliwa kwenye nafasi ya Makamu Rais, atajitahidi kupigania soka ya vijana sio tu uwepo wa vituo hai vya kukuza vipaji vya watoto, pia kuboresha mashindano mashuleni.
Anasema ufumbuzi wa soka la Tanzania ni kurejesha mfumo wa zamani wa mashindano mashuleni kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuo ambapo kijana alikuzwa kimchezo kutoka ngazi moja hadi nyingine.
Anaamini uwepo wa mashindano bora ya vijana mashuleni, utachangia kupatikana kwa vipaji vipya kila mwaka kama ilivyokuwa zamani ambapo nyota wengi walitokea kwenye mashuleni, Kombe la Taifa na timu za makampuni na mashirika.
Madega anasema uwepo wa mashindano katika shule, himizo la serikali kuwa michezo ni mahali popote pa kazi, michezo kwa ujumla wake ilishamiri kila kona ya nchi tena ikichezwa kulingana na umri.
Anasema ni kwa mfumo huo ndipo hata timu ya taifa itapata nyota bora wenye uwezo mkubwa kisoka kama ilivyokuwa zamani ambapo mchezaji aliyeitwa kikosi cha taifa, alikuwa na uwezo kamili kiuchezaji.
Ufundi
Madega anaamini ili soka iweze kupiga hatua kubwa mbele, pamoja na uwepo wa programu mbalimbali za vijana, soka ya wanawake na ile ya ufukweni, juhudi zifanyike katika uwekezaji kwenye masuala ya ufundi.
Anasema kama nchi itakuwa na makocha bora wa kutosha kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya hadi vitongoji, itasaidia kuibuliwa kwa vipaji vingi vya kufuata nyayo za kina Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Madega, mwenye uwezo na uzoefu mkubwa katika kuongoza soka akisaidiwa na taaluma ya sheria katika kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali za mchezo huo, anaamini tatizo la soka ya Tanzania sio uhaba wa vipaji, bali kukosekana kwa miundo mbinu bora na sahihi.
Madega anadokeza kuwa kwa kutambua kuwa nchi inakabiliwa na uhaba wa viwanja bora vya soka na TFF haina viwanja, akishinda atashawishi baadhi ya viwanja vikodiwe na shirikisho hilo.
“Japo najua kuna ushirikiano mzuri kati ya TFF na wamiliki, kama nitashinda nitajitahidi kushawishi kuangalia uwezekano wa shirikisho hilo kukodi viwanja hivyo ili kuviendesha na kuvisimamia vizuri,” anasema Madega.
Soka ya wanawake
Madega anasema kama ilivyo kwa wanaume, ndivyo ilivyo kwa wanawake kwani vipaji vimetapakaa kila kona ya nchi, tatizo ni kukosekana kwa mfumo bora wa kuviibua na kuviendeleza kwa maslahi yao na taifa.
Anasema kama kungekuwa na mfumo bora wa kuibua na kuendeleza vipaji vya soka ya wanawake, leo kocha wa timu ya taifa, Twiga Stars, Rogasian Kaijage, asingekuwa akiokoteza wachezaji kama anavyofanya.
“Jiulize Kaijage ni kocha wa Twiga Stars na soka ya wanawake kwa ujumla wake, anapata wapi vipaji wakati hakuna hata ligi ya soka ya wanawake?
“Vipi unawezaje kupata nyota wa kiwango cha kuchezea timu ya taifa bila kuwepo kwa mashindano? Sana sana atakachofanya kocha ni kuokoteza tu, jambo ambalo lina madhara kwa timu husika,” anasema.
Anasema tatizo hilo linaweza kupata ufumbuzi kwa kuboresha mashindano ya michezo mashuleni ikiwemo soka ya wanawake ili kupata vipaji vipya kila mwaka na kuviendeleza kwa kuwa na ligi ngazi ya wilaya hadi mkoa.
“Hili likifanyika kwa dhati, naamini soka ya wanawake itashamiri na kupata mafanikio makubwa yatakayoitangaza nchi kimataifa kwani mfumo wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika na kimataifa, si mgumu kama ilivyo kwa wanaume,” anasema.
Madega anasema kama wajumbe wa Mkutano Mkuu watamchagua katika nafasi ya Makamu wa Rais, atashirikiana na wenzake kupigania mafanikio ya soka ya vijana na wanawake akitambua kuwa soka ni ajira kwa vijana.
Kutengeneza fedha
Anasema jambo jingine ambalo atalipigania kwa kushirikiana na wenzake kama atachaguliwa ni kuhakikisha TFF inakuwa na vyanzo mbadala nje ya mapato ya milangoni na udhamini au ufadhili.
“Tunajua soka haiwezi kwenda mbele bila udhamini, ufadhili na uungwaji mkono wa wadau, lakini nje ya hayo TFF ina vyanzo gani mbadala?
“Kama nikichaguliwa, kwa nafasi hiyo nitashawishi shirikisho liwe na vyanzo vingine nje ya viingilio na wadhamini ili kujenga uwezo mzuri kiuchumi kujiendesha.
Anasema kukosekana kwa vyanzo mbadala, ndio maana Twiga Stars na timu ya wanawake wa chini ya miaka 20 iliyo kambini kwa sasa, zimekuwa zikikabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha hadi kuhitaji misaada ya wadau.
Anasema hiyo ni tofauti na ilivyo kwa timu nyingine kama Stars iliyo chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Premier Lager na mashindano ya vijana wa chini ya miaka 15 chini ya udhamini wa kampuni ya Coca Cola.
Madega anasema kama akichaguliwa atajitahidi kubuni vyanzo vipya ili kuwa na uwezo wa kuhudumia timu ambazo hazina udhamini wakati huohuo kuongeza juhudi za kusaka wadhamini wengi kadiri itakavyowezekana.
Akidokeza kuhusu miradi mbadala inayoweza kuwa chanzo cha fedha, Madega anasema ni mauzo ya jezi za timu ya taifa akiamini kama wapenzi na mashabiki watahamasishwa kwa njia mbalimbali na kufanya vizuri kwa timu husika, watanunua kwa wingi jezi za timu yao.
Anaongeza kuwa njia nyingine inayoweza kuwa chanzo cha mapato kwa TFF, ni suala la haki ya matangazo ya kurusha mechi za Stars katika televisheni mbalimbali.
Madega anaamini kama maeneo hayo mawili yatasimamiwa vizuri kwa maana ya uwajibikaji uliogubikwa na uadilifu, hata mapato yatokanayo na viingilio, yataonekana akiamini eneo hilo bado kuna matatizo.
Anasema kama TFF itajenga mazingira ya uwazi, uwajibikaji na uadilifu katika eneo hilo, ndipo chombo hicho kitazidi kuaminika mbele ya wadau na jamii, hivyo kuvutia wawekezaji zaidi katika mchezo huo.
Ushauri kwa serikali
Madega anasema kama atashinda, shirikisho hilo litaishauri serikali kupitia wizara husika kuangalia upya mahali tulipojikwaa kimichezo, ikiwezekana kuboresha zaidi mashindano mashuleni kuanzia msingi hadi sekondari.
Anakwenda zaidi ya hapo akisema, pamoja na uwepo wa mashindano katika ngazi hizo, bado hakujawa na mafanikio ya kuibuliwa kwa vipaji kama ilivyotarajiwa kutokana na changamoto mbalimbali hasa miundombinu.
Madega anasema ukifanya uchunguzi katika shule mbalimbali za msingi hadi sekondari, nyingi (hasa za mijini) hazina viwanja na vifaa vya michezo kama ilivyokuwa zamani.
“Tembelea shule za Dar es Salaam, uone kama zina viwanja…utakuta eneo ambalo lilikuwa wazi, limejengwa sekondari ya kata. Sasa jamani, hata hao watoto wanaoshiriki UMITASHUMTA na UMISSETA, wanajifunza wapi?
Anasema anavyojua, eneo la shule linapaswa kuwa si chini ya ekari 10, kwa maana ya eneo la madarasa, ofisi za waalimu, uwanja na eneo la matumizi mengine ya ardhi, lakini jambo hilo kwa sasa halipo tena.
Madega anasema kama atafanikiwa kushinda, ataketi na wenzake kwa maana ya Kamati ya Utendaji kuangalia nini wafanye akiamini yapo yanayoweza kufanywa na shirikisho hilo na mengine ni ya serikali.
Klabu
Madega anasema kama atachaguliwa, atatumia nafasi yake kuhimiza klabu kuwekeza kwenye soka ya vijana sio tu kuwa na timu ya vijana wa chini ya miaka 20, bali ikiwezekana kuanzia vijana wa kuanzia miaka sita hadi 12.
Anasema kwa vile amekuwa kiongozi wa klabu kwa miaka minne, anayajua vizuri matatizo yaliyopo katika ngazi hiyo, lakini ni jukumu la viongozi wa klabu kutambua soka ya vijana ndio siri ya mafanikio.
Udau wake katika soka
Anasema mbali ya kuipenda soka tangu akiwa mdogo na kuicheza katika ngazi ya shule ya msingi, sekondari hadi vyuoni, amekuwa kiongozi wa mchezo huo kwa muda mrefu na katika ngazi ya klabu, mkoa hadi taifa.
Mwaka 2000, alikuwa miongoni mwa maseneta wa klabu ya Yanga chini ya mfumo wa kampuni wakati huo Abbas Tarimba akiwa rais kabla ya kumwachia Francis Mponjoli Kifukwe.
Mwaka 2003, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (Corefa) na Desemba 27, 2004-2008, alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF chini ya Leodegar Chilla Tenga.
Anasema akiwa TFF, kwa kutumia taaluma yake ya sheria alishiriki kikamilifu kuhakikisha shirikisho hilo linakuwa na katiba bora na kanuni zake ambazo kwa kiasi kikubwa zimeifanya soka iheshimike.
Mei 31, 2007, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga hadi Mwaka 2010, wakati huohuo akiwa mjumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF nafasi ambayo anayo hadi sasa.
Anasema ni kiongozi pekee aliyeondoka Yanga akijivunia kuacha kiasi cha sh mil. 209, jambo ambalo limewashinda wengi ndani na nje ya klabu hiyo.
Zaidi ya fedha, Madega anajivunia kuiachia klabu hiyo alama ya biashara ya klabu hiyo (trade mark) ambayo kama itatumiwa vizuri ni chanzo cha uhakika cha mapato kwa maendeleo ya klabu hiyo mkongwe.
Madega anasema vyote hivyo vinaakisi uadilifu wake katika utendaji wa majukumu yake akiamini cheo ni dhamana na mzigo mzito wa kuwatumikia watu katika kukidhi matarajio yao, yaani mafanikio ya soka.
Wito kwa wajumbe
Madega anasema kwa vile wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, wanajua kuwa wamebeba dhamana kubwa ya hatima ya soka la Tanzania, wafanye maamuzi yatakayoipeleka soka mbele zaidi sio kurudisha nyuma ya hapa ilipo.
“Dhamana ya soka la Tanzania iko mikononi mwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
“Niseme hawa wamepata bahati kubwa ya kuibeba dhamana hiyo kwa niaba ya zaidi ya Watanzania milioni 45; Watanzania wasingependa kuona uchaguzi unatawaliwa na ushabiki,” anasema.
Madega anawasihi wajumbe wafanye maamuzi wakiongozwa na utashi wa maendeleo ya soka katika kuchagua watu wenye uwezo, weledi, uadilifu usiotiliwa shaka katika rekodi zao ili TFF ipate watu sahihi.
“Binafsi, nina imani kubwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu kwani kwa uchunguzi wangu, nimebaini ni waelewa wa mambo tena ni wenye heshima zao na elimu nzuri, hivyo wanajua wanachokifanya.