BOSI TFF AWAMWAGIA MAHELA WAAMUZI WALIOCHEZESHA SIMBA NA YANGA

Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ramadhan Nassib ametoa sh. milioni moja kwa waamuzi waliochezesha mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam. 
Nassib ambaye alichaguliwa katika nafasi hiyo akiwakilisha klabu amesema ametoa fedha hizo ili kuwapongeza waamuzi hao kwa kuchezesha vizuri mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3. 
“Waamuzi wanapofanya vibaya tunawaadhibu, hivyo wakifanya vizuri wanastahili kupongezwa pia. Vilevile kuwapongeza ni kuwaongezea ari ya kuchezesha vizuri zaidi,” amesema. 
Israel Nkongo ndiye aliyeongoza jopo hilo ambapo mwamuzi msaidizi namba moja alikuwa Hamis Chang’walu wakati namba mbili alikuwa Ferdinand Chacha. Mwamuzi wa mezani alikuwa Oden Mbaga. 
Waamuzi wote hao wana beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), na watoka Dar es Salaam ukiondoa Chacha ambaye maskani yake ni Bukoba mkoani Kagera.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)