AZAM YAIENGUA SIMBA SC KILELENI, COASTAL UNION MDONDO

Na Boniface Wambura, Ilala
BAO pekee la Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya 67 hii leo limeipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha na kupanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
Azam, imepanda kileleni baada ya kutimiza pointi 20 kutokana na mechi 10, wakiizidi pointi mbili Simba SC iliyocheza mechi tisa.
Azam kileleni Ligi Kuu; CHANZO BIN ZUBEIRY
Lakini Azam inaongoza ligi hiyo kwa wastani wa mabao tu, kwani Mbeya City iliyoifunga JKT Ruvu 1-0 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya bao pekee la Jeremiah John dakika ya 36 nayo imetimiza pointi 20, hivyo inazidiwa wastani wa mabao na timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa.
Katika mechi nyingine za leo, Ashanti United imegawana pointi na Ruvu Shooting baada ya sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Mabao ya Ashanti yalifungwa Tumba Swedi dakika ya nane kwa penalti na Mussa Nampaka dakika ya 88, wakati ya Ruvu yote yalifungwa Elias Maguri dakika za 24 na 49.
Mtibwa Sugar imeifumua 4-1 Mgambo JKT Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, mabao yake yakitiwa kimiani na Shaaban Nditi dakika ya 17, Juma Luizio dakika ya 25 na 60 na Salum Mkopi dakika ya 61, wakati la Mgambo lilifungwa na Malimi Busungu dakika ya 83.
Kagera Sugar imeilaza 1-0 Coastal Union Uwanja wa Kaitaba, Bukoba bao pekee la Salum Kanoni kwa penalti dakika ya 58.