YANGA YAPEWA SIKU 14 KUWALIPA STAHIKI ZAO, NSAJIGWA NA MWASIKA

Yanga imepewa siku 14 kuanzia leo (Septemba 13 mwaka huu) kuwalipa waliokuwa wachezaji wake msimu uliopita, nahodha Shadrack Nsajigwa na Stephen Mwasika wanaoidai klabu hiyo jumla ya sh. milioni 15.5. 
Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Septemba 12 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine ilisikiliza madai ya wachezaji hao. 
Fedha hizo ni ada ya usajili ambayo klabu hiyo ilikubaliana na wachezaji hao wakati ikiwasainisha mikataba. Yanga imeshawalipa sehemu ya fedha walizokubaliana na kiasi hicho ndicho bado hakijalipwa. Nsajigwa anadai sh. milioni 9 wakati Mwasika ni sh. milioni 6.5.