YANGA SC KUTIMKIA MBEYA KESHO

Wachezaji wa Young Africans wakishangilia bao katika mchezo dhidi ya Coastal Union mwishoni mwa mwezi uliopita

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara Young Africans leo wamefanya mazoezi ya mwisho katika viwanja vya shule ya sekondari Loyola tayari kwa safari ya kesho kuelekea Nyanda za Juu Kusini kuikabili timu iliyopanda daraja msimu huu ya Mbeya City FC siku ya jumamosi katika dimba la uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Mara baada ya kuwa na mapumziko ya wiki mbili kupisha michezo ya timu za Taifa kuwania kufuzu kwa kombe la dunia 2014 nchini Brazil, timu zote 14 zitashuka dimbani katika viwanja saba tofauti kupambana huku kila timu ikihitaji kupata pointi ili kujiweka katika mazingira mazuri. 
Young Africans itakua na michezo miwili ya Ligi Kuu mkoani Mbeya ambapo itaanza kwa kucheza na timu ya Mbeya City jumamosi septemba 14, 2013 kisha itacheza tena na maafande wa kutoka jeshi la magereza Prisons FC siku ya jumatano ya septemba 18 katika uwanja huo huo wa Sokoine.
Kocha mkuu wa Yanga mholanzi Ernie Brandts amekuwa akiendelea kukinoa kikosi chake kila siku na kuhakikisha wachezajo wake wote wanakua fit kwa ajili ya kuendelea na mikikimikiki ya kutetea tena taji la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu.
Awali wachezaji kiungo Athuman Idd 'Chuji' na mlinzi wa kati Kelvin Yondani "Cotton' walijiondoa katika timu ya Taifa ya Tanzania kufuatia kuwa majeruhi ila kwa sasa afya zao zimeimarika na wanaendelea kujifua vilivyo pamoja na wenzao katika viwanja vya shule ya sekondari ya Loyola kujiandaa na safari ya Mbeya.
Kwa mujibu wa daktari Nassoro Matuzya wa Yanga amesema wachezaji wake wote wapo fit hakuna mchezaji majeruhi hata mmoja kuelekea kwenye michezo inayowakabili hivi sasa ya nyanda za juu kusini.
Young Africans inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom ikiwa na pointi 4 baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare mmoja nyuma ya vinara maafande wa JKT Ruvu Stars  wanaongoza kwa kuwa na pointi 6 baada ya kushinda michezo yake yote.
Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuondoka kesho asubuhi kuelekea jijini Mbeya kikiwa na wachezaji wake wote waliosajiliwa kwa ajili ya kuichezea katika msimu huu,
wachezaji wanaotarajiiwa kusafiri kesho ni: 
Walinda Mlango: Ally Mustapha 'Barthez', Deogratius Munishi 'Dida' na Yusuph Abdul
Walinzi wa Pembeni: Mbuyu Twite, Juma Abdul, David Luhende na Oscar Joshua
Walinzi wa Kati: Kelvin Yondani 'Cotton', Nadir Haroub 'Cannavaro', Rajab Zahir, Ibrahim Job na Issa Ngao
Viungo Wakabaji: Athuman Idd 'Chuji', Salum Telela na Frank Domayo 'Chumvi;
Viungo Washambuliaji: Haruna Niyonzima, Nizar Khalfani, Hamis Thabit na Bakari Masoud
Washambuliaji wa Pembeni: Saimon Msuva, Mrisho Ngassa na Abdallah Mguhi
Washambuliaji wa Kati: Didier Kavumbagu, Jerson Tegete, Hussein Javu, Said Bahanuzi, Shaban Kondo na Reliants Lusajo.
CHANZO:www.youngafricans.co.tz