UCHAGUZI MKUU TASWA WANUKIA, WAANDISHI WA MICHEZO KUNOLEWA

Kama mnavyofahamu TASWA kwa kushirikiana na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) inaandaa mafunzo ya siku tano kwa waandishi wa habari za michezo nchini.
Mchakato wa mafunzo hayo bado unaendelea kwa uratibu wa karibu kati ya vyombo hivyo viwili, ambapo bado tunaendelea na mazungumzo na wadhamini mbalimbali ili kuyafanya mafunzo hayo yawe bora zaidi na mazungumzo yatakapokamilika tutawajulisha.
Kwa kuwa mafunzo hayo yatakuwa ya mara kwa mara ndiyo sababu mchakato wake unachukua muda mrefu ili pindi yatakapoanza zile ndoto zetu za kusaidia wanahabari wa michezo ziweze kutimia.   UCHAGUZI MKUU
Kamati ya Katiba ya TASWA inatarajiwa kukutana wiki inayoanza kesho kwa ajili ya masuala ya katiba ya chama chetu.
Kama mnavyofahamu chama kimekuwa na utaratibu wa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitatu na tayari muda umewadia.
Hivyo tunaamini mchakato wa katiba utaenda vizuri na baada ya kamati ya katiba kumaliza vikao vyake, Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana kwa masuala mbalimbali ikiwemo kupanga tarehe ya mkutano wa katiba na pia mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama mwaka huu.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
01/09/2013