STARS YAWASILI BANJUL, KUIVAA GAMBIA KESHO


Kikosi cha Taifa Stars kimewasili salama hapa Banjul, Gambia tayari kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji itakayochezwa kesho (Septemba 7 mwaka huu). 
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imewasili hapa jana (Septemba 5 mwaka huu) saa 11 jioni ikitokea Dakar, Senegal ambapo ilichelewa kuunganisha ndege, hivyo kuamua kutumia usafiri wa barabara kwa vile ni karibu na baadaye kupanda kivuko kuingia Banjul badala ya kulala na kuchukua ndege nyingine siku inayofuata. 
Wachezaji wako katika hali nzuri na leo jioni wanatarajia kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Independence ulioko Bakau ambao utatumika kwa mechi ya kesho. Timu imefikia hoteli ya Seaview iliyoko kandokando ya Bahari ya Atlantic. 
Mechi hiyo itaanza saa 10.30 jioni kwa saa za hapa ambapo nyumbani Tanzania itakuwa saa 1.30 usiku, na itachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda Munyemana Hudu. Waamuzi wasaidizi ni Theogene Ndagijimana, Honore Simba na Issa Kagabo. Kamishna ni Andy Quamie kutoka Liberia. 
Washabiki na vyombo vya habari vya hapa wanaizungumzia mechi hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwa pande zote, huku Gambia ikiwa imeita wachezaji tisa wanaocheza barani Ulaya na Marekani. Gambia ambayo imepata uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Gambia (GFA) imepania kuhakikisha haimalizi mechi za mchujo ikiwa na pointi moja tu. 
Kwa upande wa Tanzania, Kocha Kim Poulsen amesema nia ni kuona Stars yenye pointi sita inamaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Ivory Coast ambayo tayari imechukua tiketi pekee ya kucheza raundi ya mwisho kutoka kundi hili la C. 
“Mechi hii ni muhimu kwetu kwa vile tunataka matokeo mazuri ugenini. Lakini kikubwa ni kuwa matokeo mazuri si tu yatatuweka katika nafasi ya kuwa wa pili, lakini vilevile yatatusaidia kuongeza pointi kwenye viwango vya ubora vya FIFA, na kikubwa zaidi hii ni sehemu ya maandalizi ya sisi kucheza Fainali za Afrika za 2015,” amesema Kim. 
Stars inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja, Vincent Barnabas, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Henry Joseph, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Amri Kiemba, Mrisho Ngasa, Simon Msuva na Khamis Mcha.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
+2207362384 Banjul