PROMOTA WA PAMBANO LA CHEKA ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA KUTOMLIPA MMAREKANI

JESHI la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam limekiri kumshikilia kwa saa 24 kabla ya kumuachia kwa dhamana, promota wa pambano la ndondi la kusaka ubingwa unaotambuliwa na chama cha WBF, baina ya Francis Cheka na Mmarekani Phil Williams.
Kamanda wa polisi kanda hiyo, Suleiman Kova amewaambia waandishi wa habari hii leo kwamba walimshilia kwa muda huo promota wa mchezo huo anayejulikana kwa jina la Msangi kudaiwa kiasi cha dola 8,200 na bondia huyo wa Marekani kama sehemu ya malipo ya mpambano huo.
Alisema licha ya kumuachia  nje kwa dhamana promota huyo, bado jeshi lake linaendelea na uchunguzi wake.
Kova alisema kitendo cha kutomlipa stahiki zake bondia si tu kinautia doa mchezo huo bali nchi ya Tanzania kwa ujumla nje ya mipaka ya Tanzania.
Katika mpambano huo uliofanyika ijumaa usiku kwenye ukumbi wa Diamond Jubille jijini Dar es salaam ambapo Mtanznia Francis Cheka alifanikiwa kutwaa ubingwa.
Aidha, kabla ya kufanyika kwa mpambano huo, bondia Cheka aligoma kupanda ulingoni akitaka alipwe fedha zake na bahati nzuri alipewa fedha zake na kupanda ulingoni.