MWINYI KAZIMOTO AZIDI KUNG'ARA QATAR, KUSHIRIKI LIGI YA MABINGWA ASIA

Na Dina Ismail
NYOTA ya kiungo wa zamani wa Simba Mwinyi Kazimoto imezidi kung’ara  na huenda akashiriki ligi ya mabingwa bara la Asia , imefahamika.
Hatua hiyo inafuatia nyota huyo kuwaniwa na mabingwa wa soka wa Qatar, Al Saad ambao tayari wameshaanza mazungumzo na klabu ya Al Markhiya ya huko kwa ajili ya kumnunua nyota huyo.
Hivyo basi, kama Kazimoto atasajiliwa na Al Saad atakuwa ni mmoja ya wachezaji watakaopeperusha bendera ya Qatar katika ligi hiyo..
Habari kutoka Qatar zinaeleza kwamba, Kazimoto aliyejiunga na Al Markhiya mwezi Agosti mwaka huu amekuwa gumzo nchini humo kutokana na kiwango cha hali ya juu anachokionesha  pindi awapo dimbani.
Imeelezwa kwamba  mbali na mabingwa hao,Kazimoto pia anawaniwa na washindi wa pili wa Ligi ya Qatar, Al Gharaf hivyo kazi itabaki kwa timu yenye dau kubwa kumchukua.
Habari hizo zimeongeza kwamba, tayari  Kazimoto ameifungia mabao matatu timu yake katika mechi saba ilizocheza wakati wa ziara maalum nchini Tunisia na Oman.
“Kwa kweli kiwango cha Kazimoto kimekuwa kikiiimarika siku hadi siku kiasi ambacho viongozi wa timu kubwa wanaanza kumuwania,”alisema mtoa habari huyo
Kazimoto   amesajiliwa Al Markhiya kwa  miezi 18 kwa dau la dola 40,000.