KAMATI YA LIGI YA TFF YAPONGEZWA KWA JITIHADA ZAKE

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ameishukuru Kamati ya Ligi kwa usimamizi mzuri tangu ilipokabidhi Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) katika mzunguko wa pili msimu uliopita. 
Amesema TFF iliamua kuanzisha Kamati ya Ligi kwa lengo la kutaka klabu zijisimamie zenyewe ili kuongeza ufanisi, jambo ambalo limeleta mabadiliko kwa vile hivi sasa hakuna matatizo katika kuwalipa marefa na makamisha wanaosimamia VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL). 
“Fedha za udhamini sasa zinakwenda moja kwa moja kwenye Kamati ya Ligi. Ni matarajio yangu kuwa ufanisi utaongezeka, kwani tumeanzisha jambo hili kwa lengo la kuleta tija, maendeleo na utulivu,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na Wahariri wa Michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari. 
Rais Tenga amesema mahali penye utulivu na utawala bora watu wanakuwa na imani hasa katika masuala ya fedha, hivyo ni lazima kwa kampuni kuwekeza kwa vile kunakuwa hakuna vurugu. 
Amesema ukiondoa Afrika Kusini na Angola katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, Ligi Kuu ya Tanzania ndiyo yenye udhamini mkubwa kupitia mdhamini wa ligi na udhamini wa matangazo ya televisheni. 
Pia amesema kuanzia msimu ujao 2014/2015 klabu za Ligi Kuu hazitaruhusiwa kusajili wachezaji hadi zitakapowasilisha TFF ripoti zao za mapato na matumizi zilizokaguliwa (Audited accounts), hivyo klabu husika zijiandae kwa ripoti hizo za Januari hadi Desemba 2013. 
Kuhusu tiketi za elektroniki, Rais Tenga amesema bado linafanyiwa kazi na CRDB ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo na liko katika hatua nzuri, kwani nia ya TFF na benki hiyo kuona kuwa linaanza haraka iwezekanavyo. 
“Tiketi za elektroniki zimechelewa kuanza kwa sababu ambazo haziwezi kuzuilika, lakini CRDB imeshatengeneza miundombinu katika karibu viwanja vyote. Kulitokea uchelewaji katika kuleta printer (mashine za kuchapia), zilizokuja hazikuwa zenyewe. Kwa upande wa Uwanja wa Taifa, system (mfumo) iliyopo inatofautiana na ile ya CRDB. Hivyo sasa tunaangalia uwezekano wa zote mbili zitumike kwa pamoja, kwa sababu Uwanja wa Taifa una system yake tayari. Printer zimeshafika, tunataka ili suala lisitucheleweshe,” amesema.

Comments