Skip to main content

ILALA, KASKAZINI UNGUJA ZAANZA COPA KWA SARE

Timu za Ilala na Kaskazini Unguja zimetoka sare ya mabao 3-3 katika moja ya mechi za ufunguzi za michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 iliyoanza leo (Septemba 2 mwaka huu) katika vituo mbalimbali nchini. 
Wafungaji wa Ilala katika mechi hiyo iliyochezwa asubuhi Uwanja wa Tamco ulioko Kibaha, Pwani yalifungwa na Ally Shaban (mawili) wakati lingine lilifungwa na Haruni Said. Mabao ya Kaskazini Unguja yalifungwa na Jecha Ally (mawili) na Shehe Ally. 
Katika kituo cha Mbeya, Njombe imeanza vizuri baada ya kuifunga Katavi mabao 2-1. Mabao ya washindi yalifungwa na Rackson Mligo dakika ya 13 wakati lingine lilifungwa na Kelvin Gama dakika kumi kabla ya filimbi ya mwisho. 
Bao la Katavi katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Sekondari ya Iyunga lilifungwa dakika ya 15 kupitia Joseph Edward. 
Wenyeji Mbeya wameitandika Ruvuma mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Iyunga. Mabao ya washindi yalifungwa na Joel Mwasambungu dakika 9 wakati mengine yalifungwa na Jackson Mwaibambe dakika ya 18 na 55.  
Kesho (Septemba 3 mwaka huu) katika kituo hicho kutakuwa na mechi kati ya Rukwa na Katavi itakayochezwa saa 4 asubuhi wakati Iringa na Ruvuma zitaumana kuanzia saa 2 asubuhi.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)