BEN POL, KALA JEREMIAH NA WAKALI WENGINE KUVAMIA KAHAMA J'MOSI HII KATIKA TAMASHA LA KILI MUSIC TOUR

Msanii wa muziki wa kizazi kipya aliyejijengea heshima kubwa Tanzania Benard Paul  maarufu kama Ben Pol anatarajiwa kuungana na wasanii wengine kibao katika kupagawisha wakazi wa mji wa Kahama kwenye tamasha la ‘Kili Music Tour 2013’ tarehe 7 Septemba 2013 katika uwanja wa taifa wa Kahama.
Ben Pol anayetamba na kibao chake cha ‘Jikubali’ ni mmoja wa washindi wa tuzo za Kili Music Awards 2013 na ataungana na wasanii wengine tisa kutoa burudani ya kihistoria, “Ninachoomba kwa wakazi wa Kahama wafurike kwa wingi katika tamasha hilo ambalo tumejipanga kutoa burudani kikwetu kwetu kabisa, na itakuwa burudani ambayo haijawahi kufanyika Kahama,” alisema.
Kati ya wasanii wanaotarajiwa kuungana nae katika tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Jumamosi hii ni pamoja na Linex, Kala Jeremiah, Prof Jay, Roma Mkatoliki, Fid Q, Izzo Bizness, Recho, Lady Jay Dee na Barnaba.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa bia ya Kilimanjaro Bw George Kavishe alisema “Tunashukuru kuwa wasanii wamepokea tamasha hili kwa moyo mkunjufu kabisa na walishiriki kikamilifu kwenye mikoa yote tuliyopita na tuna ahidi kutoa burudani kali zaidi katika mikoa iliyobakia,” Alisema Bw Kavishe.
“Nafurahi sana kuona jinsi wasanii wetu wa bongo flea walivyo na vipaji vikubwa kabisa.Burudani iliyofanyika mpaka sasa ndani ya tamasha la Kili Music Tour ni la simulizi kwenye mikoa yote tuliyopita! Hii inanipa sana moyo kwamba, wasanii wamepokea tamasha hili na kuona kuwa kazi ya Tuzo za muziki za Kili ya kuendeleza vipaji imefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana,"alisema Kaviushe