WAREMBO MISS ILALA 2013 KUTAMBULISHWA IDDI PILI MANGO GARDEN HUKU TWANGA IKINGUSHA MOJA MOJA

Na Mwandishi Wetu
Bendi ya African Stars “Twanga Pepeta” itatambulisha wanamuziki wapya pamoja na warembo watakaoshiriki Miss Ilala siku ya Iddi Pili Katika ukumbi wao wa Mango Garden, Kinondoni.
Mkurugenzi wa bendi hiyo Asha Baraka alisema jana kuwa onyesho hilo limeandaliwa na Bob Entertainment na kudhaminiwa na Konyagi, Freddito Entertainment, Saluti5 na Twitter Pub.
Alisema wanamuziki watakaotambulishwa siku hiyo maalum ni wanenguaji wapya, muimbaji Ige Moyaba ambaye alikuwa mwanamuziki wa bendi hiyo kabla kwenda Ufaransa kuendeleza kipaji chake.
 “Tumeamua kuleta wanenguaji wapya kabisa, wenye damu changa ili kuleta mapinduzi kwenye muziki wa dansi. Madansa wetu ni mabinti warembo, pia tuna wanenguaji watanashati,” alisema Asha na kuongeza kuwa awameamua kubadilisha wanenguaji ili kuenda na wakati pamoja na soko la muziki.
Kwa upande wa Ige Moyaba aliyetamba kwenye albamu ya ‘Mtu Pesa’ katika mwaka wa 2004,  Asha alisema ameanda vitu vipya kuwapa mashabiki wa bendi hiyo inayotamba kwa staili ya Kisigino.
“Kwa kweli hi siyo onyesho la kukosa kwani itakuwa ni zawadi yetu ya Idd kwa mashabiki wetu,” mkurugenzi huyo alisema.
Mwezi uliyopita Twanga Pepeta walizindua albamu yao ya 10 lijulikanayo kana “Nyumbani ni Nyumbani”.
Albamu zingine ambazo zitapigiwa siku hiyo ni Jirani, Fainali Uzeeni, Chuki Binafsi, Ukubwa Jiwe, Mtu Pesa, Safari, Password, Mtaa Wa Kwanza, Mwana Dar es Salaam na Dunia Daraja.
Naye mratibu wa onyesho hilo Joseph Kapinga alisema kuwa warembo watakoshiriki kwenye shindano la kumtafuta Redds Miss Ilala pia watatambulishwa siku hiyo.