WACHEZAJI COASTAL UNION KULAMBA 500,000 KILA MMOJA IWAPO WATAIFUNGA YANGA

KATIKA kuongeza morali kwa wachezaji wake, uongozi wa klabu ya Coastal Union ya Tanga umetangaza bingo ya shilingi 500,000 kwa kila mchezaji iwapo watafanikiwa kuwafunga mabingwa watetezi wa Ligi kuu bara Yanga Sc.
Timu hizo zinatarajiwa kukutana jumatano katika mchezo wa pili wa liugi hiyo iliyoanza kutimua vumbi Agosti 24.
Mwenyekiti wa Coastal Union Hemed Aurora amesema kwamba lengo la kutangaza bingo hiyo ni kuongeza ari kwa wachezaji wake ili kuweza kukabiliana kwa nguvu zote na wapinzani wao na hatimaye kushinda.
"Hii ni kama kuongeza morali kwa wachezaji wetu kwani Yanga ni timu kubwa  na fedha hizi si kwa wale watakaocheza tu bali hata kwa wale watakakuwa benchi,"alisema.
Aliongeza kuwa kikosi chake kipo katika hali nzuri baada ya kufanya vema katika mchezo wake wa fungua dimba dhidi ya maafande wa JKT Oljoro uliopigwa katika dimba la Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Mchezo baina ya timu hizo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwani kila timu ityahitaji kushinda ilui kuondoka na pointi tatu muhimu.
Katika mchezo wa kwanza Yanga iliitandika Ashanti united mabao 5-1, huku Coastal iliibanjua JKT Oljoro mabao 2-0.