TIKETI MECHI YA YANGA, AZAM KUUZWA ASUBUHI

Tiketi kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam itakayochezwa kesho (Agosti 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitaanza kuuzwa saa 3 asubuhi. 
Vituo vitakavyouza tiketi hizo Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Barber Shop iliyoko Sinza Madukani. 
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari yote yanayouza tiketi yatahamia uwanjani saa 7 kamili mchana. 
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya VIP C watalipa sh. 15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A watalipa sh. 30,000. 

COCA COLA YATOA MIPIRA 100, FULANA 800
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa kampuni ya Coca Cola kwa kukabidhi fulana 800 na mipira 100 kwa ajili ya ngazi ya mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya mikoa yanayoanza Septemba Mosi mwaka huu. 
Coca Cola ndiyo inayodhamini mashindano hayo yaliyoanzia ngazi ya wilaya ambapo mwaka huu yatachezwa kwa kanda na baadaye fainali itakayochezwa kuanzia Septemba 7-14 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishirikisha mikoa 16 itakayokuwa imefanya vizuri katika ngazi ya kanda.
Kila mkoa utapata fulana 25 na mipira mitatu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu zao kwa ajili ya michuano hiyo ngazi ya kanda itakayomazika Septemba 6 mwaka huu. 
Kanda hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha. 
Zanzibar itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke na mkoa mmoja wa Unguja.

Comments