TFF YAOMBOLEZA KIFO CHA MWANDISHI ABM RADIO

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari za michezo wa Radio ABM ya Dodoma, Gracemo Bambaza kilichotokea Agosti 14 mwaka huu katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam. 
Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani Bambaza kwa kipindi chote akiwa mwandishi alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo mchango wake katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima. 
Bambaza aliyezaliwa mwaka 1973 na ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika vituo vya redio vya Wapo cha Dar es Salaam na Pride cha Mtwara amesafirishwa jana (Agosti 15 mwaka huu) kwenda Karagwe mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi. 
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Bambaza, ABM Radio na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. 
Mungu aiweke roho ya marehemu Bambaza mahali pema peponi. Amina