TAMBWE, KAZE KUTAMBULISHWA UWANJA WA TAIFA J'2 KWA MCHEZO DHIDI YA MAFUNZO

NYOTA wa kimataifa wa Simba Amisi Tambwe na Gilbert  Kaze kutoka Burundi wanatarajiwa kutambulishwa rasmi jumapili hii kupitia mchezo wa kirafiki baina ya Simba na Mafunzo inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Huo utakuwa mchezo wa kwanza kwa wachezaji hao ambao pia wanakipiga katika timu ya Taifa ya Burundi ‘Intamba Murugamba’kukichezea kikosi cha Simba jijini dar es Salaam tangu kujiunga nayo kwa ajili ya kuichezea kwenye msimu wa ligi wa 2013/2014.
Katibu Mkuu wa Simba  Evodius Mtawala ameiambia SPORTS LADY BLOG  kwamba mchezo huo ni maalum kwa ajili ya kuwatambulisha wachezaji hao baada ya kushindwa kufanya hivyo katika tamasha la Simba Day.
Alisema mchezo huo ni zaidi ya mechi ya kirafiki kwani utasaidia kukiweka sawa kwa namna moja ama nyingine kikosi cha Simba ambacho kinaendelea na michezo yake ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara iliyoanza mkutimua vumbi juzi iliyopita.
Hata hivyo wachezaji hao walishindwa kuichezea Simba kwa sababu ya kutokuwa na hati za uhamisho wa Kimataifa (ITC) kabla ya mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage kufunga safari hadi Burundi na juzi kurejea nazo na hivyo kufanya wachezaji hao kuwa tayari kuichezea timu yao katika  michezo itakayofuata.

Mtawala aliongeza kuwa kikosi cha Simba ambacho kipo njiani kwa ajili ya kuelea mjini Arusha tayari kwa mchezo wake wa ligi kuu bara dhidi ya wenyeji JKT Oljoro utakaopigwa keshokutwa  kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Mchezo baina ya Simba na Oljoro utakuwa wa pili ambapo katika mchezo wa awali wa ligi hiyo ililazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Rhino ya Tabora, mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Comments