TAMASHA LA KILI TOUR LAFANA NDANI YA JIJI LA MWANZA

Na Mwandishi Wetu
Tamasha la muziki la Kilimanjaro ambalo liko kwenye ziara nchi nzima kuhamasisha watanzania kujivunia bidhaa za nyumbani, lililopachikwa jina la kikwetukwetu, mwishoni mwa wiki hii lilivunja rekodi mkoani mwanza ambapo mashabiki zaidi ya 10000 walifurika katika viwanja vya CCM Kirumba na kushuhudia wasanii zaidi ya 10 wakubwa wakitawala jukwaa kwa kutoa burudani na kushukuru mashabiki kwa kuwaunga mkono kwa kusikiliza muziki wao.
Ziara hiyo ambayo ilisimama kwa muda kupisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, imeanza rasmi tena wiki hii mkoani mwanza ambapo wiki ijayo inatarajiwa kuhamia kwenye mji wa Kahama ikiwa na wasanii wakubwa katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya, ambao pamoja na kiuiwashukuru mashabiki wao na kutoa burudani, pia watakuwa wakihamasisha watanzania wenzao kujivunia vya nyumbani.
Meneja wa bia ya Kilimanjaro, ambao ndio wadhamini wakubwa wa ziara hiyo ameliambia gazeti hili kwamba huu ni mkoa wa nne kwa ziara hii kupita ambapo kabla ya mwezi wa Ramadhani, tamasha lilipita katika mikoa ya Tanga, Moshi na Dodoma ambapo matokeo yalikuwa ya hali ya juu kama ilivyokuwa kwa Mwanza.
"Ziara hii huwa ni ya kila mwaka, ila ina utofauti kidogo mwaka hyuu. Mwaka jana tulikuwa tunachukua washindi wa tunzo za Kilimanjaro tu, lakini mwaka huu tumeamua kuchukua wasanii mchanganyiko wenye mvuto na kuzunguka nao ili kutumia muziki kuhamasisha kuhusiana na watanzania kujivunia bidhaa zao", alisema Kavishe.
Mkoani Mwanza, wasanii waliofanya onesho ni Dabo, Snura, Ben Pol, AT, Kala Jeremiah, Bob Junior, Diamond, Profesa Jay, Fid Q, Lady Jaydee na Roma Mkatoliki.
kwa mujibu wa Kavishe, orodha za wasanii huenda zikawa zinabadilika kila mkoa kutokana na mvuto wa msanii katika mkoa huo, hivyo orodha hii hubadilika mara kwa mara.
"kwa mfano Kahama tutakuwa na MwanaFA ambaye huku hayupo kabisa na pengine tusiwe na Roma Mkatoliki na Snura labda, tukaweka wengine", alifafanua Kavishe.