SIMBA YAMTOSA KAZIMOTO, YASEMA OFA YA KUMNUNUA NI UPUUZI MTUPU

SIMBA imekataa ofa iliyotolewa na klabu ya Al Markhiya ya Qatar kwa ajili ya kumsajili aliyekuwa kiungo wake, Mwinyi Kazimoto kwa madai kuwa ni ndogo sana ukilinganisha thamani ya mchezaji huyo.
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alikiri kwamba wamepokea ofa kutoka timu ya moja ya Qatar lakini ni ofa ndogo sana ambayo hawawezi kuikubali kwani thamani yake haifikii ile waliyomuhamishia kutoka JKT Ruvu. 
Hata hivyo, Kamwaga alisema hawezi kuzungumzia kwa undani juu ya suala la Kazimoto kutokana na ukweli kwamba bado ana maswali ya kujibu Watanzania na klabu yake ya Simba kwa ujumla. 
“Suala la Kazimoto tumeliweka pembeni kwani tunatarajia kukaa na TFF kwa ajili ya kumjadili na baada ya hapo mambo mengine kuhusu yeye yatafuata,”alisema 
Ikumbukwe kuwa, Kazimoto alitimkia Qatar hivi karibuni baada ya kutoroka katika kambi ya timu ya Taifa siku ambayo ilikwaanza na Uganda ‘The Cranes’ katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika zinazoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN). 
Kazimoto aliyesajiliwa na Simba kutoka JKT Ruvu alikwenda kujaribiwa na klabu ya Al Markhiya Sc inayoshiriki Ligi daraja la kwanza ya huko na kufuzu na hivyo wakala wake, Mahmoud Abu Al Ght kuwasiliana na uongozi wa Simba kwa ajili ya ofa hiyo.


Comments