SIMBA KUKIPIGA NA SC VILLA YA UGANDA AGOSTI 10


TIMU ya soka ya Simba inatarajiwa kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi SC Villa ya Uganda mchezo utakaopigwa Agosti 10 katika Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ni maalum kwa klabu ya Simba kuadhimisha miaka 77  tangu kuanzishwa kwake ambapo tayari klabu hiyo imeanza kufanya kazi mbalimbali za kijamii.
Katibu Mkuu wa Simba Evodius Mtawala amesema kwamba maandalizi kwa ajili ya mchhezo huo utakaohitimishwa baada ya tamasha maalum yanakwenda vizuri ambapo Villa watatua nchini keshokutwa.
Alisema kupitia mchezo huo pia mashabiki wa Simba watapata fursa nyingine ya kuwashuhudia baadhi ya nyota wake wapya waliosajili na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara pamoja na michuano mingine.
“Pia katika tamasha hilo litakaloambatana na burudani mbalimbali, tutatambulisha jezi zetu mpya tutakazozitumia katika msimu ujao wa ligi,”alisema Mtawala.
Baadhi ya nyota wapya waliosajiliwa Simba ni pamoja na Mrundi Amisi Tambwe, Waganda Joseph Owino na Gilbert Kaze na wazawa kama Abdulhalim Homoud, Betram Mombeki na wengineo.

Simba kwa sasa ipo kambini kwenye hoteli ya Bamba Beach iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam ikiendelea na maandalizi yake chini ya makocha Abdallah Kibaden ‘Mputa’ akisaidiwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

Comments