RUVU SHOOTING KUJIPIMA NA MABINGWA WA MKOA WA PWANI KESHO UWANJA WA MABATINI

TIMU ya soka ya Ruvu Shooting ya mkoani Pwani kesho inatarajiwa kujitupa katika uwanja wa wake wa nyumbani wa Mabatini kwa ajili ya kujipima ubavu mabingwa wa soka mkoa wa Pwani, Kiluvya United. 
Ofisa habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire alisema jana kwamba mchezo huo utakaoanza saa 10 jioni ni sehemu ya maandalizi ya timu yake kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 24. 
Alisema mchezo huo ni muhimu sana kwao kwani kocha mkuu wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa atapata kuona mapungufu yaliyoipo ili aweze kuyafanyia kazi mapema kabla ya kuanza kwa ligi hiyo. 
“Kocha anatarajia kuwachezesha wachezaji wote hususani waliosajiliwa msimu huu ili kuwa na uhakika wa uwezo na nafasi wanazozimudu kuzicheza,”alisema 
Ruvu Shooting ni miongoni mwa timu za Ligi kuu zilizosajili vizuri kwa lengo la kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika ligi hiyo kwa kutoa ushindano mkubwa na hatimaye kufanya vizuri katika michezo yake. 

Baadhi ya wachezaji wapya iliyowaongeza ni pamoja na Cosmas Ader, Juma Nade, Elias Maguli, Juma Seif ‘Kijiko’, Lambele Jerome, Stephano Mwasyika na Abdul Seif Juma.