RUVU JKT YAANZA VIBAYA LIGI KUU YA NETIBOLI

TIMU ya netiboli ya Ruvu JKT ya Kibaha mkoani Pwani imeanza vibaya ligi Kuu ya mchezo huo baada ya kuchapwa magoli 21-14 na Jeshi Star ya Dar es Salaam katika michuano hiyo iliyoanza jana mkoani Mbeya.
Katika mchezo huo uliofanyika asubuhi ya jana, Ruvu JKT mbali  na kucheza vema walijikuta wakizamisha jahazi kutokana na wafungaji wake kukosa umakini na utulivuwalipopata nafasi ya kufunga.
Ilimlazimu kocha wa JKT ruvu inayomilikiwa na kikosi cha 832 KJ, Argentina Daud kufanya mabadiliko kwa kumbadili Anita Elias kutoka nafasi ya ulinzi (GD) na kumpeleka ufungaji(GA), huku akimtoa Ashura Sadick (GA) na kumuingiza Leons Augustino (GD).
Kocha Argentina pia alimtoa mlinzi wa pembeni (WD) Monica Peter na kumuingiza Fatuma Ally, lakini mabadiliko hayo hayakuzaa matunda.
Timu hiyo leo inatarajiwa kutupa karata yake ya pili kwa kuumana na Polisi Arusha na kisha baadaye Filbert Bayi ya mkoani Pwani.
Msemaji timu hiyo Masau Bwire alisema pamoja na timu yake kufanya vibaya katika mchezo wa awali bado ana matumaini ya timu yake kufanya vema katika michezo inayofuata na kuibuka na ubingwa wa michuanio hiyo na hasa ikizingatiwa kwamba kikosi chao kinaundwa na wachezaji wenye viwango vya hali ya juu.

Comments