Skip to main content

NITAMSHANGILIA FRANCIS CHEKA KATIKA PAMBANO LAKE LA UBINGWA WA DUNIA

Na Onesmo Ngowi, Rais wa IBF/Africa 
Katikati ya miaka ya 90, nchi ya Tanzania ilipata bahati ya kuwa na bingwa wa ngumi wa dunia ambaye alitambuliwa na Umoja wa Ngumi wa Dunia (WBU). Rashid Matumla aliweza kuonyesha dunia kwamba Tanzania pia inaweza kushindana na kushinda katika medani ya ngumi za kulipwa hivyo aliweza kujizolea sifa kemkem yeye binafsi pamoja na nchi yetu ya Tanzania.  Ilikuwa ni miaka ya msisimko kwenye ngumi za kulipwa na wadau pamoja na mabondia wengi walisisimka na uwezekano wa nchi yetu kuweza kushinda mataji mengi zaidi ya Afrika, Mabara pamoja na dunia. 
Wakati Rashidi akiwa bingwa wa dunia, mdogo wake Mbwana naye alikuwa bingwa wa mabara alietambuliwa na WBU pia. Hiyo iliongeza chachu na hamasa kwa wadau wa ngumi za kulipwa hivyo nchi ilikuwa kwenye shamrashamra za aina ya pekee. 
Mkuzaji (Promota) aliyefanya mambo yote hayo si mwingine bali ni Kampuni ya DJB Boxing Promotions iliyokuwa inamilikiwa na kuendeshwa kwa umahiri na ndugu wawili Dionis Malinzi na Jamal Malinzi. Ndugu hawa wazalendo kweli waliweza kuwekeza kiasi kikubwa sana katika kuwaendeleza  kina Matumla pamoja na mabondia wengine wengi hapa Tanzania.  Ni Watanzania wachache alioweza kushiriki au kuwekeza katika michezo kama kina Malinzi na hiyo iliweza kuitangaza nchi yetu kwa kiasi kikubwa. 
Kina Malinzi hawakuwaandalia tu mapambano kina Matumla bali walienda mbali na kuwapeleka nchini Afrika ya Kusini ili waweze kufanya mazoezi kwenye gyms zilizokwa na vifaa vya kisasa pamoja na wataalamu mahiri waliowafanyia mazoezi na kubadili kabisa uwezo wao wa kupigana kuwa wa hali ya juu kama mabondia wezngie katika nchi zilizoendelea. 
Tanzania imepita katika kipindi kirefu na kigumu bika kuweza kuwa na msisimko kama ule ambao kina Matumla chini ya kina Malinzi waliuleta nchini. Pamoja na kwamba Magoma Shabani kutoka Tanga alikuja pia kuwa bingwa wa dunia aliyetabuliwa pia na WBU lakini ule msisimko waliouleta kina Matumla na kima Malinzi ulishafifia.

Ujio wa bondia Francis Cheka na wengine wa jika lake umeanza tena kufufua matumaini na msisimko wa ngumi za kulipwa hapa Tanzania. Cheka bondia kutokaMorogoro ameweza kuwa kivutio pekee wa ngumi za kulipwa kwa sasa hapa Tanzania na Afrika ya Mashariki kwa ujumla. 
Francis Cheka ni bondia pekee katika bara la Afrika ambaye ameweza kushinda na kutetea taji la IBF kwa kipindi kirefu. 
Nikiwa kama Rais wa IBF katika bara la Afrika,Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, ninaona faraja kubwa sana kuwa karibu na bondia Francis Cheka. Kwa kweli umahiri wake sio tu kwenye ulingo bali ni namna Cheka anavyojichanganya na watu wengine katika jamii. 
Francis Cheka anatambuliwa kuwa bondia namba 4 katika viwango vya mabara vya IBF na ni bondia pekee katika bara la Afrika aliye na kiwango cha juu kama hicho katika orodha ya mabondia wa kiafrika katika uzito wake wa Super Middle. 
Tanzania imeona na kushughudia malumbano mengi katika ngumi za kulipwa ambayo yanaletwa na sababu ambazo hazina msingi.  Tumefikia mahali tumalize tifauti zetu na kukaa meza moja ili tuweze kuuendeleza mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini kwa faida ya taifa letu ili kuwapata kima Matumla na kina Cheka wengi zaidi. Pia ushirikiano wetu utawapa moyo kina Malinzi wengi zaidi kuweza kushirikiana katika kuuendeleza mchezo wa ngumi. 
Nataka itambulike rasmi kuwa bondia ana HAKI ya kuchagua ni taji lipi au chama kipi anataka kupigania. Chaguo lake lisilete mzozo au vivu kati ya wanaosimamia mchezo wa ngumi badala yake ulete ushirikiano utakaoweza kumsaidia bondia mwenyewe ili aweze kushinda na kuitangaza nchi yetu vizuri. 
Ndiyo maana naona faraja sana kwa bondia Francis Cheka kupata nafasi ya kupigana pambano la dunia. Kwangu mimi Francis Cheka ni bingwa wangu wa Afrika (IBF) mpaka atakapopanda ulingoni siku ya tarehe 30 Augusti katika ukumbi ya Diamond Jubilee. Mimi itakuwa mmoja wa maelfu ya Watanzania watakaokwenda katika ukumbi ule kumshangilia Francis Cheka akiipeperusha bendera ya Tanzania.
Kwa kawaida bingwa wa shirikisho moja akishaamua kuwania mkanda wa shirikisho lingine anapoteza ubingwa wa shirikisho alilokuwa analishikilia. Lakini nimechukua pia jukumu la kuhakikisha kuwa kwa bahati mbaya kama Cheka akishindwa kuupata ubingwa wa dunia hatapoteza ubingwa wake wa IBF Afrika. Pia hatapoteza viwangio vyake alivyonavyo katika IBF. Hii itamsadia kuweza kung’ara zaidi.
Mimi nadhani imefikia wakati sasa sisi watanzania wenye nia nzuri ya maendeleo kushirikiana na kuhakikisha kuwa nchi hii inapiga hatua kwenye medani ya ngumi.
Hongera Sana Francis Cheka pamoja na waandaaji wa mpambano huo muruwa.

Comments