MWAKIBINGA: MAJIMAJI KAMPUNI ITAKUWA MFANO KUONDOA UBABAISHAJI SOKA LA BONGO

Damas, Ndumbaro mmoja ya wadau wa soka waliodhamiria kuifufua Majimaji
Aliyepata kuwa Mkurugenzi wa Fedha TFF na Mtaalamu wa masuala ya fedha, hisa na kodi Bwana Silas Mwakibinga amesema kuwa mfumo wa Majimaji Kampuni na kuingizwa kwenye soko la hisa kutakuwa mfano kwa klabu za Tanzania kuona jinsi ambavyo ubabaishaji unaweza kumalizwa kwenye soka.
Bwana Mwakibinga amesisitiza kuwa ili ubabaishaji uishe katika mpira wa Tanzania ni lazima iwepo klabu ya mfano na Majimaji FC inachokifanya kuingia kwenye Kampuni na hisa zake kuuzwa ndio kile ambacho Watanzania wanakitaka.
“Unajua vilabu vyetu vimekuwa na ubabaishaji kutokana na kukosa mfumo unaoeleweka. Lakini Majimaji FC Kampuni na kuingia kwenye soko la hisa kutalazimisha kutoa mapato na matumizi kwa mujibu wa sheria ya soko la hisa kila mwezi jambo ambalo tayari linaondoa ubabaishaji wowote ule.” Alisema Mwakibinga.
Aidha Mwakibinga amewataka wafadhili mbalimbali ambao wanataka kuwekeza kwenye soka kujiandaa kuweka fedha zao Majimaji kwakuwa watapata taarifa zote za uendeshaji wa klabu kwa mujibu wa sheria.
“Sheria itailazimisha Majimaji kutoa mapato na matumizi lakini vilabu vingine vinaingia kwenye migogoro kwa sababu hakuna utaratibu huo kwao na hawalazimishwi na sheria.” 
Tayari wadau mbalimbali wamekwishathibitisha kushiriki katika Majimaji Revival Conference, mkutano wa kujadili mfumo na mikakati ya kiuendeshaji ambayo itajengwa kwaajili ya Majimaji FC Kampuni itakayozaliwa tarehe 10 Agosti 2013 katika ukumbi wa Centenary chini ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mh. Said Mwambungu.
Pamoja na Silas Mwakibinga mtoa mada mwingine katika Majimaji Revival Conference anatarajiwa kuwa Dkt Damas Ndumbaro, Mwanasheria na wakala wa kimataifa wa FIFA.


Comments