KUZIONA YANGA, COASTAL UNION KESHO BUKU TANO TU

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya pili kesho (Agosti 24 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani huku macho na masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Yanga na Coastal Union.
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna atakuwa Omari Walii kutoka Arusha.
Mtibwa Sugar itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakuwa mwenyeji wa pambano kati ya wenyeji Rhino Rangers na Azam.
Vumbi lingine litatimka kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati maafande wa JKT Ruvu watakapokwaruzana na wenzao wa Tanzania Prisons kutoka Mbeya. Mbeya City na Ruvu Shooting zitacheza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Jiji la Tanga litakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ashanti United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Oljoro JKT itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.