CAF YAMTEUA KAMISHNA RWIZA KUSIMAMIA MECHI YA CHAN

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Alfred Rwiza wa Tanzania kuwa kamishna wa mechi ya raundi ya pili ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Rwiza atakuwa kamishna katika mechi ya kwanza ya raundi hiyo itakayohusisha mshindi wa mechi kati ya Msumbiji na Namibia dhidi ya Angola itakayochezwa kati ya Agosti 9 na 11 mwaka huu. Mechi hiyo itachezeshwa na refa Noram Matemera kutoka Zimbabwe.
Matemera atasaidiwa na Wazimbabwe wenzake Tapfumaney Mutengwa atakayekuwa mwamuzi msaidizi namba moja, Ncube Salani ambaye ni mwamuzi msaidizi namba mbili wakati mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Ruzive Ruzive.