YANGA WAMGEUZIA KIBAO KIIZA, WAAMUA KUTAFUTA MSHIRIKA WA KAVUMBAGU

Na Dina Ismail
BAADA ya kuipiga danadana kwa muda mrefu, hatimaye klabu ya soka ya Yanga imemgeuzia kibao aliyekuwa kiungo mshambuliaji wake wa kimataifa,Hamis Kiiza. 
Hivi karibuni nyota huyo kutoka nchini Uganda, amekuwa katika mvutano na uongozi wa klabu hiyo juu ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kutumikia klabu hiyo. 
Kwamba, Kiiza alitaka kuongezwa ofa ya aliyopewa na uongozi kutoka dola 35,000 hadi dola 50, 000 ambazo amesisitiza kupewa na baadaye kumuongeza hadi dola 40,000. 
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zinaeleza kwamba wameamua kuachana kwanza na suala la Kiiza kutokana na nafasi yake kutokuwa na umuhimu katika kikosi hicho. 
Kiongozi mmoja aliliambia gazeti hili kwamba kwa sasa Yanga inahitaji mshambuliaji halisi mmoja ambaye atashirikiana na mshambuliaji aliyepo sasa, Didier Kavumbagu. 
“Kwa sasa suala la Kiiza tumeliweka kando kwani nafasi yake haina umuhimu katika kikosi chetu, tunatafuta mshambuliaji halisi, ila tukikosa ndo tutarudi kwake,”alisema 
Akienda mbali zaidi, kiongozi huyo alisema kwamba mshambuliaji huyo anafahamu kila kitu juu ya mustakabali wake ndani ya klabu hiyo na hata hilo suala la kumpa fedha anayoitaka yeye halipo. 
Aliongeza kuwa baada ya kumleta mshambuliaji kutoka Nigeria Ogbu Brendan  kwa ajili ya majaribio, hivi karibuni tena wanataleta washambuliaji wengine kuja kujaribiwa. 
Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga kimeendelea na mazoezi yake ya kujiandaa na ligi kuu soka Tanzania Bara ambapo keshokutwa itacheza mechi ya kirafiki na URA ya Uganda. 

Mchezo huo utakaopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kukipima kikosi hicho.