WAJUMBE MKUTANO MKUU MAALUMU WA TFF WAANZA KUWASILI


Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika kesho(Julai 13 mwaka huu) wanatarajiwa kuanza kuwasili jijini Dar es Salaam leo, imefahamika.
Mkutano huo wa marekebisho ya Katiba utakuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga na utafanyika ukumbi wa NSSF Waterfront kuanzia saa 3 kamili asubuhi. Wajumbe wote wa mkutano huo watafikia hoteli ya Travertine.
 Pia mkutano huo utahudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa wakiwemo kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).

MECHI YA STAND, KIMONDO NAYO KUPIGWA JUMAPILI
Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Stand United FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya Mbeya iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) imesogezwa mbele kwa siku moja.

Timu hizo sasa zitacheza Jumapili (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Kimondo ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na Polisi Jamii ya Mara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Mwamuzi wa mechi hiyo ni Hans Mabena kutoka Tanga.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)