Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi
kutoka Madagascar kuchezesha
mechi kati ya Tanzania
(Taifa Stars) na Uganda (The
Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa Mandela ulioko
Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala .
Waamuzi wataongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi
msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba
mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno
akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official).
Kamishna wa mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya mwisho
kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ni
Ismail Kamal kutoka Ethiopia .
Mechi hiyo namba 38 itachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni
kwa saa za Afrika Mashariki. Taifa Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa
Julai 13 mwaka huu jijini Dar es
Salaam kwa bao 1-0.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko
kambini jijini Mwanza ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya
hizo mbili itacheza Fainali za CHAN mwakani nchini Afrika Kusini.
Comments
Post a Comment