SIMBA, URA WATUA LEO, KUZIONA J'MOS BUKU TANO TU

WAKATI  kikosi cha  timu ya soka ya URA ya Uganda kikitarajiwa kuwasili nchini leo tayari kuzivaa klabu kongwe za Simba na Yanga mwishoni mwa wiki hii, kiingilio cha chini cha mechi baina yao na Simba kimepangwa kuwa sh.5,000. 
Simba na URA zinatarajiwa kukwaana keshokutwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku kiingilio hicho kitahusisha mashabiki watakaokaa viti vya kijani, bluu na orange. 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, George Wakuganda alisema kwamba wameamua kuweka viingilio vya hali ya chini ili kutoa fursa kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo. 
Alivitaja viingilio vingine ni shilingi 15, 000 kwa watakaokaa VIP B  na shilingi 20,000 kwa watakaoketi VIP A. 
Wakuganda aliongeza kuwa maandalizi kwa ajili michezo hiyo yanakwenda vema huku lengo la michezo hizo pamoja na kuvipima vikosi vya timu hizo, pia ni sehemu ya utambulisho ya wachezaji wapya watakaozitumikia timu hizo katika msimu mpya wa Ligi Kuu Soka Tanzania  Bara utakaoanza mwezi Agosti. 
Alisema  kikosi cha URA kinatarajiwa kuja na nyota wake wote wakali hivyo anaamini makocha wa Simba na Yanga watapata fursa nzuri ya kujua viwango vya wachezaji wao kupitia michezo hiyo. 
Naye Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kwamba kikosi cha Simba kilichokuwa kwenye ziarta maalum ya kimichezo katika mikoa ya Tabora, Katavi na Mara kinatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo. 

Kamwaga alisema kikosi chao kipo vizuri na tayari kwa mchezo huo na hasa ikizinmgatiowa kuwa ziara waliyoifanya huko imewapa mazoezi ya kutosha hivyo mashabiki wasubiri kuona timu ikiibuka na ushindi.