RAIS KIKWETE MGENI RASMI TAMASHA LA MATUMAINI LITAKALORINDIMA U/TAIFA JULAI 7

Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Matumaini ambalo litafanyika keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa tamasha hilo, Abdallah Mrisho, amesema Rais Kikwete ambaye hivi karibuni alikuwa na ugeni mkubwa wa Rais wa Marekani, Barack Obama, amekubali kuwa mgeni rasmi ambapo atatoa neno la matumaini kwa maelfu ya watu watakaojitokeza uwanjani hapo.

Eric Shigongo.
Akizungumzia zaidi juu ya ugeni huo mkubwa, Mrisho alisema: “Rais Kikwete amekubali ombi letu la kuwa mgeni rasmi, atatumia nafasi hiyo kutoa neno la matumaini kwa wote watakaojitokeza uwanjani hapo.
“Rais pia ndiye atakayefungua mechi ya Wabunge wa Simba dhidi ya Yanga ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa. Kama ujuavyo rais wetu ni mtu wa watu na ni mpenda michezo, hilo linajulikana siku zote.”

Rais Kikwete.
Aidha, Mrisho aliongeza kwa kusema kuwa shabaha ya tamasha hilo ni kuamsha upya imani ya Watanzania kwa nchi yao. Kuwafanya wawe wazalendo na kila mmoja kujiona analo jukumu la kufanya, kuhakikisha Tanzania yetu inapiga hatua.
“Mbali na Rais Kikwete, wengine watakaotoa neno la matumaini siku hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers Ltd, Eric Shigongo.

Zitto Kabwe.
“Wengine ni Mwenyekiti wa Taasisi ya East Africa Speakers Bureau Limited (EASB), Paul Mashauri, mwalimu wa kimataifa wa ujasiriamali, James Mwang’amba na mwanamitindo, Jokate Mwegelo.
“Wote hao, kila mmoja atakuwa na fursa ya kufikisha Neno la Matumaini ili kila atakayehudhuria Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, aondoke akiwa mpya, akiwa na matumaini mapya kwa taifa lake na maisha yake kwa jumla,” alisema Mrisho.

Nape Nnauye.
Kwa upande wake Shigongo amesema kuwa udini, ukabila na kila aina ya ubaguzi, vitachimbiwa shimo na kuzikwa.
“Taifa linapita kwenye kipindi kigumu ambacho ni changamoto nzito. Unazungumzwa ufisadi, migomo imekuwa mingi, udini na ukabila vinapenyezwa kwa kasi, pamoja na aina zote za ubaguzi, hivi vyote tunapaswa kuvizika.
“Tuna makusudio ya kuwafanya Watanzania wajione wamoja licha ya tofauti za kiitikadi zilizopo. Mahitaji yetu ni kupaza sauti kuwa kila mtu yupo huru kusimamia anachokiamini lakini linapokuja suala la umoja wa kitaifa, tofauti zote zinapaswa kuwekwa kando,” alisema Shigongo.

Paul Mashauri.
Akizungumzia juu ya tamasha hilo, Shigongo alisema: “Hivi karibuni matokeo ya kidato cha nne yalitoka hapa nchini na kuonyesha watoto wengi walikuwa wamefeli. Kilichoniuma zaidi ni niliposikia baadhi ya watoto waliamua kukatisha maisha yao kwa sababu matokeo yao yalikuwa mabaya.”

Comments