NGOMA INOGILE YA UDE UDE KUZINDULIWA SIKU YA EID EL FITR CLUB BILICANAS


MSANII wa bongo fleva Hamidu Hafidh Mshinda maarufu kama Ude Ude anatarajia kuzindua rasmi video ya wimbo wake uitwao Ngoma Inogile, siku ya Idd Mosi katika ukumbi wa kimtaifa wa Club Bilicanas. 
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, msanii huyo alisema maandalizi kwa ajili ya uzinduzi huo yanakwenda vema, hivyo amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kula. 
Alisema singo hiyo iliyotayarishwa katika studio za Fire Music chini ya mtayarishaji More Fire ameshaisambaza kwenye vituo mbalimbali vya redio tangu juzi  ambapo anamini wataipokea vema kazi yake hiyo mpya. 
“Tayari singo nimeshaisambaza kwenye vituo mbalimbali vya redio tangu jumatatu, nawaomba mashabiki wangu muipokee kwa mikono miwili, pia msikose kuja kushuhudia uzinduzi wa video yake sikukuu ya Iddi Mosi pale Club Bilicanas,”alisema. 

Ude Ude ni mmoja ya wasanii wenye vipaji vya aina yake ambapo awali alipata kutoka na singo kadhaa zilizomtambulisha katika muziki huo zikiwemo Kujinafasi, Nipe kidogo na nyinginezo.