MAKALA:MWANZO NA MWISHO WA KASEJA SIMBA SC

 Na Dina Ismail
HIVI karibuni mlinda mlango namba moja Tanzania, Juma Kaseja amepata kuwa gumzo katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.
Gumzo hilo linatokana na uongozi wa timu ya soka ya Simba kutangaza kutomuongeza mkataba wa kuendelea kuichezea klabu hiyo baada ya kuitumikia kwa karibu miaka tisa.
Uongozi wa Simba uliamua kuvunja ukimya kwa kutangaza kutomsaini tena Kaseja baada ya kuwepo sintofahamu iliyokuwa ikiendelea ndani ya klabu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika mwezi Mei.
Kwamba, viongozi wa Simba waligawanyika makundi mawili kuhusiana na suala la Kaseja, ambaye alikuwa pia nahodha wa timu hiyo ambapo kuna waliotaka aongezwe mkataba na kuna waliotaka asiongezwe.
Ilifikia hatua hata vikao vyao kuvunjika baada ya suala la Kaseja kuibuka, kwani viongozi walijikuta katika mabishano na mwisho wa siku kushindwa kupatikana mwafaka.
 Hata hivyo hakukuwa na sababu ya msingi ya viongozi hao kugawanyika na hasa katika suala la kutomtaka tena katika klabu yao zaidi ya kutoa sababu zisizo na mashiko yoyote.
Kingine ni kwamba, hata kocha mkuu wa timu hiyo Abdallah ‘King’ Kibaden  naye alipigilia msumari juu ya mustakabali wa Kaseja na kusema kuwa asingekuwa tayari kuifundisha Simba iwapo Kaseja angeongezwa mkataba.
Kibaden naye alikataa uwepo wa Kaseja ndani ya kikosi chake bila ya kutoa sababu, kama ni kuwa ameshuka kiwango, mtovu wa nidhamu au lingine lolote.
Sakata hilo lilikuwa likichukua sura mpya kila kukicha, wapo waliodai Kaseja kutaka dau kubwa ili kusaini mkataba mpya, wapo waliodai nyota huyo anataka mkataba wa miaka miwili wakati uongozi unataka kumpa mwaka mmoja, lakini katika hilo uongozi ulidai kuwa haujaketi chini kuzungumza na Kaseja juu ya hayo.
Kuachwa kwa Kaseja haikuwa jambo la kushitukiza hata kidogo bali ni mkakati uliopangwa kwa muda mrefu na hatimaye kuhitimishwa katikati ya wiki hii.
Kila mpenda soka hapa nchini anafahamu kiwango alicho nacho Kaseja na yaliyokuwa yakitokea hapa katikati, inawezekana ni kughafirika kulikotokana na kuchanganywa na hali tete iliyokuwa ikimuandama ndani ya klabu yake.
Kaseja ni mmoja ya wachezaji wachache sana wanaoithamini kazi yao na ubora wake ulianza kuonekana tangu alipokuwa sekondari ya Makongo, timu za Vijana kabla ya kusajiliwa na timu za Ligi Kuu ameweza kulinda kiwango chake kwa kiasi kikubwa.
Tofauti na wachezaji wengine, Kaseja amekuwa ‘Tanzania One’ kwa muda mrefu na alikomaa zaidi katika namba hiyo baada ya kustaafu kwa aliyekuwa ‘Tanzania One’ Mohammed Mwameja na kurithi nafasi yake ndani ya Simba tangu mwaka 2003.
Kaseja pia amekuwa chaguo namba moja katika kikosi cha timu ya Taifa tangu akizichezea timu za vijana hadi ile ya wakubwa na ni mara chache sane makocha walishindwa kumpanga katika kikosi cha kwanza.
Lakini Kaseja alianza kuonekana si lolote baada ya timu yake ya Simba kuanza kufanya vibaya katika ligi kuu bara na michuano ya kimataifa misimu miwili iliyopita na ndipo jina lake lilianza ‘kunuka’.
Kwa wenye kumbuku nzuri, Kaseja pamoja na baadhi ya wachezaji waliokuwa katika kikosi hicho kwa muda mrefu kama Mussa Hassan Mgosi, Mohammed Banka, Victor Costa, Haruna Moshi ‘Boban’,  na wengineo walisukiwa mpango wa kuondolewa kundini.
Haikuwa kwa hao tu bali mkakati huo uliwahusu hata baadhi ya wachezaji wengine ambao walihamia katika timu hiyo kama Amir Maftah, Juma Nyoso, Mwinyi Kazimoto na wengineo  huku ikidaiwa kutaka kuondoa wakongwe kwani kwa wakati huo Simba iliweka mkakati wa kuwatumia vijana zaidi.
Kwamba wachezaji hao wamekuwa ‘virusi vibaya’ ndani ya timu hivyo kuendelea kuwa nao italeta athari kwa wachezaji chipukizi ambao walianza kuonesha ustawi mzuri ndani ya Simba.
Na ndipo walianza kuondolewa mmoja baada ya mwingine baada ya kusimamishwa kwa muda usiojulikana kwa madai ni watovu wa nidhamu (kwa sababu mbalimbali) na kupotezewa mpaka mkataba kuisha.
Wengine walipelekwa kucheza kwa mkopo katika vilabu mbalimbali mradi tu waondoe virusi, lakini kwa Kaseja ilishindikana kwani hawakupata sababu ya kumtoa kafara kabla ya zamu yake kufika wiki iliyopita baada ya ‘kuvuliwa gwanda’ lake.
Baada ya uongozi kutangaza rasmi kuachana naye, ndipo ikabainika kwamba, chanzo ni mechi ya funga dimba ya ligi kuu bara dhidi ya mahasimu wao Yanga ambapo Simba ilitandikwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Mei 18 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Taarifa za ndani kutoka Simba zinadai kuwa, Kaseja aliihujumu Simba na matokeo yake timu ilipoteza mchezo huo ambapo yeye alikaa langoni.
Kwa  mantiki hiyo, kitendo kile kiliwaudhi sana viongozi kwani mabao aliyofungwa yalionekana dhahiri kuwa yalitokana na uzembe wake kwani kwa umahiri alionao isingekuwa rahisi nyavu zake kutikiswa siku hiyo.
Kiongozi mmoja wa Simba alisema kwamba pamoja na  mapungufu yote aliyonayo Kaseja lakini walikerwa  zaidi na kufungwa kwake.
“Hivi unavyomfahamu wewe Kaseja anaweza kufungwa mabao kama yale, kwa kweli hilo limetacha na maswali mengi kichwani, imetkera sana mwache aende zake,”alisema
Akienda mbali zaidi, kiongozi huyo alisema ingekuwa vizuri zaidi kama Kaseja angeweza kuonesha umahiri wake na kuondoa dhana mbovu dhidi yake, lakini kitendo cha kukubali nyavu zake kutikiswa kilitoa jawabu juu ya maswali walitokuwa nayo.
Hilo ndilo lilihitimisha mjadala juu ya sababu ya kutemwa kwa Kaseja ndani ya klabu hiyo aliyochezea kwa mafanikio tangu alipojiunga nayo mwaka 2003 akitokea Moro United.
Hata hivyo, Kaseja ambaye si mzungumzaji sana wa vyombo vya habari ameendelea kukaa kimya juu ya suala lake hili na jitihada za kumtafuta ziligonga mwamba baada ya kukataa kuzungumza lolote.
“Dada nakuheshimu sana, lakini kwa sasa sipo tayari kuzungumzia suala langu na Simba au soka kama una lingine uliza,” alisema Kaseja kwa simu kutoka kwao Kigoma alipokwenda kwa mapumziko.

HUYU NDIYE JUMA KASEJA
Alizaliwa Aprili 20, 1985 huko Kitongoni, Ujiji mkoani Kigoma akiwa mtoto wa nne katika Familia ya marehemu Mzee Kaseja.
Amekuwa akiupenda mpira wa miguu tangu akiwa mdogo akirithi kipaji cha marehemu baba yake ambapo anasema alipata kucheza miaka ya zamani na baba mzazi wa mchezaji wa Simba ambaye sasa ni kocha wa timu ya Vijana ya Simba, Suleiman Abdallah Matola.
Alianza kucheza tangu shule ya msingi  hivyo kuchaguliwa katika mashindano ya Taifa (UMITASHUMTA) ambapo huko ndipo alipong’ara na Mkuu wa Shule ya Sekondari Makongo wakati huo, kanali Idd Kipingu alimchagua Kaseja pamoja na wachezaji toka sehemu wengvine na kuwapeleka shuleni hapo kwa ajili ya kuendeleza viopaji vyao.
Baada ya kusukwa kwa karibu miaka minne, alipata nafasi ya kuichezea Taifa ya vijana wenye umri wa miaka 17 kabla ya kipaji chake kuwavutia viongozi wa timu ya Moro United na kuichezea mwaka 2001 hadi 2002.
Mwaka  2003 mpaka 2008 aliichezea Simba kabla ya 2009 kujiunga na mahasimu wao Yanga alipodumu nayo kwa mwaka mmoja ambapo pia aliiwezesha kutwaa ubingwa wa msimu huo kabla kurejea tena Simba alipoichezea hadi mwishoni mwa msimu huu.
Mbali na soka Kaseja pia anajihusisha na usajiliamali ambapo anamiliki duka la nguo lililopo maeneo ya Msasani  liitwalo KASEJA Classic Wear.