KUELEKEA MKUTANO SIMBA SC KESHO:WANACHAMA WATAKA MABADILIKO KATIKA BAADHI YA VIPENGELE VYA KATIBA


WAKATI mkutano mkuu wa wanachama wa klabu ya Simba ukitarajiwa kufanyika kesho katika Bwalo la maofisa wa Polisi Oyesterbay jijini Dar es Salaam, baadhi ya wanachama wameomba kufanyika kwa mabadiliko katika baadhi ya vipengele vilivyomo kwenye  Katiba ya klabu hiyo ili kuendana na wakati. 
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake, Daniel Kamna (100) amesema kwamba, lengo la kutaka mabadiliko hayo ni kuendana na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa soka hapa dunaini kwa mujibu wa Mashirikisho ya soka ikiwemo la kimataifa  (FIFA),  Afrika (CAF) na Tanzania (TFF). 
Alivitaja vipengele hivyo ni pamoja na Ibara ya 26 inayohusu sifa za wagombea ambapo kifungu cha tano kinasomeka kuwa;mwanachama akitiwa hatiani kwa kosa la jinai asigomnee nafasi yoyote katika klabu hiyo na wao kuomba mabadiliko hayo yasomeke:asiwe ametiwa hatiani kwa kosa la jinai lenye adhabu ya kifungo cha zaidi ya miezi sita bila mbadala wa faini katika miaka mitatu iliyopita. 
Kamna aliongeza kuwa, mabadiliko mengine wanayoomba ni baadhi ya majina ya vyeo ya viongozi ambapo badala ya Mwenyekiti aitwe Rais, Makamu Mwenyekiti aitwe Makamu wa Rais. 
“Pia mkutano mkuu wa uchaguzi uwe na mabadiliko yafuatayo kwa viongozi wa kuchaguliwa wawe ni Rais na  Makamu wa Rais”, alisema 
Aliongeza kuwa katika kipengele cha kamati ya utendaji;Ibara ya 28 inayozungumzia muundo, wameomba isomeke kwamba:Kamati ya utendaji ya Simba Sports Club itaundwa na Rais, Makamu wa Rais, Wajumbe saba ikiwemo mwanamke mmoja wa kuteuliwa na Rais na mjumbe mmoja wa kuteuliwa akitokea Baraza la Wazee.