KOZI YA SOKA LA UFUKWENI KUFUNGULIWA LEO JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga atakuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa kozi ya mpira wa miguu wa ufukweni (beach soccer) itakayoanza leo jijini Dar es Salaam. 
Kozi hiyo itafanyika kwa wiki nzima kwenye klabu ya Escape iliyoko karibu na Safari Carnival, Mikocheni karibu na makao makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)- JKT Mlalakuwa. Uzinduzi utafanyika saa 3 kamili asubuhi. 
Washiriki wa kozi hiyo itakayokuwa chini ya wakufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ni 60 ambapo 30 ni makocha wa mpira wa miguu na 30 wengine ni waamuzi wa mpira wa miguu. 
Wakufunzi hao wa FIFA ni Angelo Schirinzi kutoka Uswisi kwa upande wa makocha wakati George Postmar kutoka Uholanzi ndiye atakayewanoa waamuzi.