KIJIKO AIBUKIA RUVU SHOOTING,SIMBA NA YANGA ZAMKOSA DILUNGA

JUHUDI za Klabu za Yanga na Simba katika  kumfukuzia mshambuliaji mahiri Hassan Dilunga wa  timu ya Ruvu Shooting ya Pwani, zimeingia dosari baada ya nyota huyo kuongezewa mkataba.
Mbali ya kufanikiwa kumbakisha Dilunga, Shooting pia imemsajili kiungo Juma Seif ‘Kijiko’ aliyewahi kuichezea Yanga kabla ya kuhamia kwa mkopo African Lyon ambayo imeshuka daraja.
Kijiko anaungana na nyota mwingine kinda, Cosmas Ader, aliyekuwa akiwaniwa na timu kadhaa zikiwemo kongwe za
Simba na Yanga.
Kabla ya kutua Shooting, Ader alikuwa kicheza kwa mkopo Lyon akitokea klabu ya Azam FC.
Ofisa habari wa Shooting, Masau Bwire ameiambia Sports Lady kwamba kuwa, wamekamilisha usajili wa nyota wa msimu ujao wa 2013/14.
Alisema usajili limefanyika kwa umakini ili kuwa na kikosi bora kitakacholeta ushindani mkubwa kwenye  ligi hiyo inayotazamiwa kuanza Agosti 24.
“Tunashukuru kwa kiasi kikubwa, tumefanikisha usajili wa kikosi chetu kulingana na mahitaji ya timu, naamini tutatoa ushindani mkubwa kwenye msimu ujao,” alisema.

Nyota wengine waliosajiliwa Shooting na timu zao kwenye mabano, ni Jerome Lambele (Azam) aliyekuwa akicheza kwa mkopo Ashanti United na  Juma Nade (Kagera Sugar).