KIIZA AENDELEA KUIKOMALIA YANGA SC

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Yanga, Mganda Hamis Kiiza, ameendelea kuuweka njia panda uongozi wa klabu hiyo kutokana na msimamo wake wa kutaka dau kubwa ili aweze kusaini mkataba mpya.
Uongozi wa Yanga, ulimtangazia dau la dola 35,000 za Marekani nyota huyo ili asaini, lakini aligoma kwa madai kuwa ni ndogo, ukilinganisha na mchango mkubwa anaoutoa ndani ya klabu hiyo.
Habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, zinaeleza kwamba, licha ya uongozi kujaribu kuzungumza naye, lakini nyota huyo ameendelea kuwa na msimamo huo.
Imeelezwa kuwa, Kiiza bado ana nafasi ndani ya kikosi hicho na hasa ikizingatiwa kuwa, ni mmoja wa wachezaji ambao kocha mkuu, Mholanzi Ernie Brandts, amependekeza wawepo msimu ujao.
Hata hivyo, msimamo wake wa kutaka dau kubwa, huenda ukampotezea nafasi ndani ya klabu hiyo, kwani uongozi umesisitiza kuwa, hauna fedha zaidi ya hiyo.

Kiiza ambaye alijiunga na Yanga Julai 2010, kwa sasa yupo kwao nchini Uganda.