KAZIMOTO AFUZU MAJARIBIO QATAR, AIANGUKIA SIMBA

KLABU ya Al Markhiya Sports Club ya Doha, Qatar imetuma barua kwa uongozi wa Simba ukiomba umruhusu kiungo wake Mwinyi Kazimoto kujiunga na timu hiyo baada ya nyota kufanya vizuri katika majaribia yake hivi karibuni.
Habari za uhakika zinasema, Kazimoto aliyekwenda Qatar wiki iliyopita kusaka nafasi ya kucheza soka la kulipwa katika klabu hiyo, ameshafanyiwa vipimo vyote hivyo kinachotakiwa ni kibali tu kwa ajili ya kuichezea timu hiyo iliyoasisiwa mwaka 1995 ambayo sasa inacheza Ligi Daraja la Pili.
Japo nyota huyo aliondoka bila idhini ya viongozi wa Simba wala wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kutokana na kuondoka nchini akitokea kambi ya timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars,  Al Markhiya imeiangukia Simba kuomba ridhaa yake.
Tanzania Daima ilipoutafuta uongozi wa Simba kuhusu jambo hilo, kiongozi mmoja wa Simba alikiri kuwepo kwa barua hiyo iliyoandikwa na Mohamed Abu Ali, lakini wenye mamlaka juu ya uamuzi huo ni viongozi wa juu wa klabu.
“Kweli kuna hiyo kitu, lakini siwezi kulizungumzia kwa undani zaidi kwani sina uamuzi juu ya hili na hasa ikizingatiwa mazingira ambayo mchezaji mwenyewe aliondoka sasa tuwaachie viongozi wenye mamlaka,”alisema
Hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa juu wa  Simba aliyeweza kupatika jana baada ya kutopokea simu zao za viganjani.

Kama Kazimoto atapata baraka kutoka kwa uongozi wa Simba atakuwa ni miongoni mwa nyota wa Tanzania wanaopata ulaji wa kutakata kupitia soka la kulipwa.

Comments