HII NI RASMI :KAZIMOTO ONDOKA JANA KWENDA QATAR

KIUNGO wa Simba Mwinyi Kazimoto ameondoka nchini jana jioni kwenda Doha,  Qatar kucheza soka la kulipwa, imefahamika. 
Awali kulikuwa na taarifa kwamba nyota huyo aliondoka nchini jumapili iliyopita lakini vyanzo vya kuaminika viliiambia Sports Lady Blog kwamba Kazimoto aliondoka jana (Alhamis) baada ya kutumiwa viza na wenyeji wake.
"Ilikuwa aondoke jumanne lakini viza yake ilikuwa haijatumwa hivyo ameondoka jana jioni,"kiliongeza chanzo hicho.
Kazimoto ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ anakwenda huko kujiunga na timu moja inayoshiriki Ligi daraja la Kwanza. 
Habari za uhakika zilizopatikana jana zinaeleza kwamba nyota huyo anakwenda huko baada ya klabu hiyo kuvutiwa na kiwango cha mchezaji huyo na hivyo kufanya mchakato wa kumpeleka huko. 
Imeelezwa kwamba, kabla ya kusajiliwa rasmi kiungo huyo atafanyiwa majaribio na iwapo atafuzu atasaini mkataba mnono ambapo utampatia kitita kinono. 
Hata hivyo, inadaiwa kwamba Kazimoto amekwenda huko bila ridhaa ya uongozi wa klabu yake ya Simba wala timu ya Taifa ambayo alikuwa nayo kambini kabla ya kutoweka ghafla baada ya mchezo wao na Uganda ‘The Cranes’ uliopigwa jumamosi iliyopita kwenye uwanja wa Taifa na Stars kuchapwa bao 1-0. 
Kazimoto aliyejiunga na Simba mwaka juzi akitokea JKT Ruvu, inadaiwa kwamba ameamua kwenda kujaribu bahati yake huko baada ya kuona hali si shwari kwa upande wake katika klabu ya Simba.