DULAYO KUPAGAWAISHA TANGA SIKUKUU YA IDD

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Abdulrahaman Kasembe ‘Dulayo’, anatarajia kufanya onesho la aina yake kwa ajili ya kuwapagawisha mashabiki wake Mkoani Tanga katika Sikukuu ya Iddi El Fitri.
Katika onyesho hilo ambalo litafanyika katika maeneo mawili tofauti, Dulayo ataambatana na wasanii mbalimbali kwa ajili ya kutoa burudani safi.
Ziara hiyo ambayo imeandalikwa na SG Entertainment, siku ya Iddi Mosi itafanyika kwenye Ukumbi wa Chuo Cha Ualimu cha Korogwe ambapo Iddi Pili atamalizia Pangani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Dulayo alisema kuwa onyesho hilo litakalofanyika Tanga ni kwa ajili ya kuizindua nyimbo yake mpya ya Mara Mia, ambayo imerekodiwa hivi karibuni na kuanza kufanya vizuri katika vituo mbalimbali vya Redio nchini.
Alisema kuwa pia atatoa zawadi kwa mashabiki wake kwa kuwaimbia nyimbo mbalimbali zilizopo kwenye albamu yake ikiwa ni pamoja na Twende na Mimi, Mida ya Kazi, Bila Yule pamoja na Hawalali.
Alisema kuwa katika onyesho hilo ataambatana na wasanii mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ommy G, Mon G, P The MC pamoja na Salu B.
Dulayo alisema kuwa pia wanatarajia kusaka vipaji katika onesho hilo na msanii chipukizi atakayeshinda, atakuja Dar es Salaam kwa ajili ya kurekodi wimbo mmoja na mchana kutakuwa na shoo kwa ajili ya watoto. 
“Nimeandaa shoo ya aina yake kwa mashabiki wangu na hivyo ninatarajia kuwa watafurahia kutokana na kuwaandalia vitu vipya” alisema.