DIDA, ZAHIR WAANZA KUJINOA YANGA


Dida akiwa mazoezini jana asubuhi uwanja wa shule ya Sekondari Loyola
Mlinda mlango mpya aliyesajiliwa na mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara Deogratius Munishi 'Dida' pamoja mlinzi wa kati aliyekua akiichezea timu ya Mtibwa Sugar msimu uliopita Rajab Zahir jana wameanza rasmi mazoezi na timu yao ya Young Africans Sports Club kwa ajili ya msimu mpya 2013/2014.
Deogratius Munishi 'Dida' ameungana na wachezaji wengine wawili mshambuliaji Shaban Kondo aliyekua akicheza soka nchini Msumbiji pamoja na mlinzi wa kati Rajab Zahir aliyerejea kutoka nchini Afrika Kusini alipokuwa akifanya majaribio katika timu mbili za Ligi Kuu nchini humo.
Mapema jana katika siku ya kwanza ya mazoezi kiungo mshambuliiaji Mrisho Khalfani Ngasa alifanya mazoezi asubuhi chini ya kocha mholanzi Ernest Brandts kabla ya kocha huyo kuwapa nafasi wachezaji wote wa timu ya Taifa kujiunga na timu leo kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Uganda julai 13 Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Mpaka sasa klabu ya Yanga imefanikiwa kusajili wachezaji watano ambao ni:
1. Deogratius Munishi 'Dida' - Huru (Azam)
2. Rajab Zahir - Huru (Mtibwa)
3. Mrisho Ngassa - Huru (Azam)
4. Shaban Kondo  -  Huru
5. Realitus Lusajo - Machava FC
Kocha Brandts amefurahia kuongezeka kwa wachezaji hao kwani amesema atapata fursa ya kukaa nao na kucheza michezo ya kirafiki kanda ya ziwa hali itakayopelekea kupata nafasi ya nzuri kukiandaa kikosi na msimu mpya wa 2013/2014.
Yanga itaendelea na mazoezi leo asubuhi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ziara yake  kanda ziwa inayotazamiwa kuanza mwishoni mwa wiki jijini Mwanza.
Wachezaji wote wameendelea na mazoezi leo asubuhi isipokua wachezaji waliojiunga na kambi ya timu ya Taifa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Uganda
Rajab Zahir akiwa mazoezini uwanja wa shule ya Sekondari Loyola jana asubuhi.
Na www.youngafricans.co.tz