KOCHA WA YANGA BRANDTS KUTUA LEO, MAZOEZI KUANZA KESHO


MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara timu ya Yanga kesho inatarajiwa kuanza mazoezi rasmi kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi hiyo pamoja na michuano ya kimataifa.
 Ofisa habari wa Yanga Baraka Kizuguto amesema kwamba kikosi cha timu hiyo kitakuwa kikifanya mazoezi yake katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola- Mabibo jijini Dar es salaam.
 Alisema mazoezi hayo yatakuwa chini ya kocha mkuu Mholanzi Ernie Brandts ambaye anatarajiwa kuwasili usiku wa leo akitokea kwao alipokwenda kwa mapumziko mafupi. 
Kizuguto alisema timu hiyo itafanya mazoezi yake jijini kwa siku tatu mfululzio kabla ya siku ya ijumaa kusafiri kuelekea jijini Mwanza kwa ajili ya ziara maalum ya kimichezo itakayoambatana na shamrashamra za kupeleka ubingwa wa ligi hiyo kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa. 
Alisema siku ya Jumamosi timu hiyo itashuka katika dimba la CCM Kirumba kukwaanma na mabingwa wenzao wa Uganda, Kampala City Council (KCC), kabla ya kurudiana Jumapili mjini Shinyanga, mchezo utakaopigwa dimba la Kambarage. 
“Baada ya michezo hiyo, jumatatu timu itaelekea mjini Tabora kwa ajili ya mchezo mmoja wa kirafiki ambao utapangwa na waandaaji na kisha kikosi kitarejea jijini Dar es salaam kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa ligi,”alisema.