APR, GOR MAHIA ZAMPIGIA CHAPUO KASEJA

KLABU za APR ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya zipo katika harakarti za kumwania aliyekuwa kipa namba moja wa timu ya Simba, Juma Kaseja, imefahamika.
Habari za uhakika ambazo Sports Lady Blog imezinyaka  zinasema viongozi wa timu hizo wameshaanza mazungumzo na Kaseja ili kumsajili kwa msimu ujao katika nchi hizo.
Mdau mmoja wa soka ambaye yupo karibu na uongozi wa timu hizo, alidokeza jana kwamba, kwa nyakati viongozi wa timu hizo mbili, wamekuwa kwenye harakati za kumsaka Kaseja, wakiamini bado ni kipa mwenye uwezo mkubwa langoni.
Licha ya kutemwa kwenye kikosi cha Simba kwa msimu ujao, Kaseja bado kipa namba moja wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars chini ya kocha wake Kim Poulsen, raia wa Denmark.
Habari zaidi zinasema, klabu ya APR iliyofika fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashabiki na Kati-Kagame Cup na kufungwa na Vital’o wiki moja iliyopira nchini Sudan, inapewa nafasi kubwa ya kumpata kipa huyo.
Hayo yanatokea huku Kaseja akiwa kwenye kambi ya timu ya Stars inayojiandaa na mechi ya kuwania tiketi ya Fainali za Afrika kwa Nyota wa Ndani –CHAN dhidi ya Uganda itakayopigwa Julai 13, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
“Ujue baada ya Simba kutangaza kuachana na Kaseja, kuna timu nyingi hasa za nje zimeonesha nia ya kutaka kumsajili lakini mpaka sasa ni APR na Gor Mahia ndio wako makini zaidi na mchakato huo,” kilisema chanzo hicho.
Hivi karibuni uongozi wa Simba ulitangaza kuachana na Kaseja aliyekuwa kipa wake namba moja na nahodha wa timu hiyo bila ya kuweka rasmi sababu za kuachana naye baada ya kumaliza mkataba wake, Meii.

Aidha, baadhi ya klabu za Ligi kuu ambazo zilikuwa zikitajwa kumuania nyota huyo aliyeitumikia Simba nazo zilidai hazina mpango wa kumsajili kwani zinamakipa wa kutosha.

Comments