ABDALLAH KIBADENI:TURUFU MUHIMU YA MAKOCHA WAZALENDO LIGI KUU 2013/2014


Na Dina Ismail
MSIMU  wa 2012/2013 wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara ulikuwa mbaya kwa Simba ambayo ilikabiliwa na mithani ya hapa na pale, lakini kubwa lilikuwa ni kupokwa ubingwa wa ligi hiyo na mahasimu wao, Yanga.
Dalili za kupoteza ubingwa huo zilianza kuonekana tangu mzunguko wa kwanza baada ya timu kutokuwa na matokeo ya kuridhisha huku kocha mkuu wa wakati huo, Milovan Cirkovic, akiahidi neema baadaye lakini hali haikuwa hivyo.
Ndipo uongozi ukaamua kumfuta kazi Milovan na kumuajiri kocha Mfaransa Patrick Liewig ambaye aliichukua timu katika mzunguko wa pili wa Ligi hiyo, lakini matokeo yake naye hakuweza kufua dafu na mwisho wa siku, Simba ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu.
Baada ya kumalizika kwa ligi hiyo uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wake Alhaj Ismail Aden Rage ulijaribu kuangalia mustakabali mzima wa benchi la ufundi la timu hiyo na ndipo ulipoamua kumpa jukumu hilo kocha mzawa, Abdallah ‘King’ Kibaden.
Kibaden ambaye alikuwa akiinoa klabu ya Kagera Sugar si mara yake ya kwanza kuifundisha klabu ya Simba, kwani amekuwa akifanya hivyo kwa nyakati tofauti.
Ikumbukukwe kuwa Simba imepata katika makocha tofauti wazawa wakiwemo Athuman Juma Kalomba, Mohammed Kajole, marehemu Syllersaid Mziray na wengineo.
Lakini kwa zaidi ya miaka 10, ni Mziray ndiye aliyeweza kuipatia mafanikio.
Simba ilipitia kipindi kigumu katika tangu mwaka 1997  kabla ya  mwaka 2001.
Ilipopata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Washindi na hilo liliwezeshwa chini ya Mziray.
Hivyo, Kibaden ambaye pia kwenye mlolongo wa makocha wazawa waliopata kuitumikia Simba yumo katika orodha, kwa sasa ana deni kwa mashabiki wa Simba la kuhakikisha anarudisha historia ya marehemu Mziray.
Hilo linawezekana kwani kwa uwezo na uzoefu wa Kibaden, kama atapewa ushirikiano atarejesha matumaini ya mashabiki wa Simba kwa timu yaliyoanza kupotea tangu mwaka 2011 kwa timu kufanya vibaya katika mechi zake.
Kwamba, Kibaden ana uzoefu mkubwa na ufundishaji na hasa ikizingatiwa kuwa katika timu alizopata kuziongoza, kiwango cha wachezaji kilikuwa cha kuridhisha sana na hatimaye kuony
esha ushindani mkubwa katika michezo yake.
Simba imempa jukumu hilo Kibaden baada ya kuwa na imani naye kubwa sana, ambapo anaifanya kazi hiyo akisaidiwa na mzawa mwenzake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Tangu ajiunge na Simba mwezi Mei mwaka huu, Kibaden amekuwa katika mkakati mkubwa wa kuhakikisha anaipatia mafanikio timu hiyo ndani na nje ya nchi.
Aidha kwa kuonyesha kuwa wazawa wanaweza, Kibaden ameonyesha kutaka kutoa nafasi zaidi kwa wachezaji wa Tanzania akiamini kwamba wana vipaji na uwezo mzuri isipokuwa hawapewi nafasi uwanjani.
Kama hiyo haitoshi, Kibaden amesema anahitaji zaidi wachezaji wanaojituma uwanjani sambamba na kuwa na nidhamu ambayo ni jambo la muhimu kwa wachezaji katika mafanikio yao ya uwanjani.
Kwa sasa Simba iliyoanza kuonyesha uhai, imekuwa katika maandalizi yake ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Agosti hivyo ndio hapo mashabiki watakapoanza kutaka kuona mafanikio ya kocha huyo.


HISTORIA

Kibadeni alizaliwa Oktoba 11, 1949 jijini Dar es Salaam ambapo akianzia kucheza soka tangu akiwa mdogo.
Mwaka 1969, alijiunga na Simba (wakati huo Sunderland) akitokea Kahe Republic ya Mtaa wa Kongo na Mchikichi, Kariakoo.
Mwaka 1974 alilifunga bao la pili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Hearts Of Oak ya Ghana nchini Ghana katika Robo Fainali ya Kwanza ya Klabu Bingwa Afrika, kabla ya kuing’oza Simba kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika hadi sasa.
Mwaka 1975 aliiongoza Simba kuwa ya kwanza kubeba Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, michuano ambayo ilichezwa jijini Dar es Salaam.
Mwaka 1977, Kibadeni, aliifungia Simba mabao matatu peke yake katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Yanga SC.
Mwaka 1978 aliondoka Simba na kwenda kuwa kocha mchezaji wa Majimaji ya Songea na kuing’arisha vilivyo.
Mwaka 1993, aliiwezesha Simba kufika Fainali ya Kombe la CAF akiwa kocha, rekodi ambayo haijavunjwa hadi leo ikiwa ni miaka 20 baadaye.
Kibaden ni muumini mzuri wa dini ya Kiisalmu ambapo mwaka 2011 alikwenda Hijja.
Safari hii ametua Simba akitokea Kagera Sugar alikoipatia nafasi ya nne katika Ligi Kuu, akiwa na mkakati wake maalumu katika usajili kwa nyota wa kigeni.
Kibadeni aliyeibuka Kocha Bora wa Ligi Kuu katika msimu huu, amekuwa akisajili mchezaji kwa uwezo wake dimbani si umaarufu wa jina au kwa vile anatoka nje.
Hata hivyo, Kibadeni anakabiliwa na mtihani mgumu wa kudhihirisha ubora na nafasi ya makocha wazawa katika soka la Tanzania kwani ametua Simba akichukua nafasi ya Milovan Cirkovic raia wa Serbia.
Hiyo ni kutokana na ukweli kuwa kwa vile Simba ni miongoni mwa klabu tatu bora nchini, huku akiwa mzalendo pekee katika kapu hilo, ni nafasi yake kuonesha uwezo dhidi ya Ernie Brandts (Yanga) na John Stewart Hall (Azam).
Ni wazi Kibadeni ana nafasi ya kudhihirisha uwezo wa makocha wazawa katika soka ya Tanzania kutokana na ukweli kuwa ni muda mrefu Yanga na Simba zimekuwa chini ya makocha wa kigeni.
Ndivyo ilivyo pia kwa Azam ambayo tangu ianze kucheza Ligi Kuu, haijawahi kunolewa na mzalengo kama kocha mkuu wake, isipokuwa kutoka Uingereza na Ureno.
Namaliza kwa kusema sina hofu na uwezo wa Kibadeni katika ufundishaji kwani mbali ya uwezo na uzoefu, ni kocha anayewajua vizuri wachezaji wa Tanzania na Ligi Kuu kwa ujumla. Kila la kheri.