WADAU WAANZA KUUNYOOSHEA KIDOLE MKUTANO MKUU WA TFF

LICHA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutetea Mkutano Mkuu wa Julai 13 kugongana na mechi ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa nyota wa Ligi za Ndani (CHAN), suala hilo limeonekana kugeuzwa nongwa na baadhi ya wadau.
Jana, baadhi ya wadau walihoji mantiki ya mkutano mkuu kugongana na mechi hiyo kwa hoja kuwa, mechi hiyo ingeweza kupisha mkutano huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na uzito wa agenda zinazotakiwa kujadiliwa ikiwemo uundwaji wa Kamati ya Maadili.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alitetea jambo hilo akisema ni kitu cha kawaida kwani suala la mechi lipo chini ya sekretarieti ya shirikisho hilo ambayo haihusiki na mkutano huo isipokuwa wajumbe wa mkutano mkuu.
Pamoja na ufafanuzi huo, wadau wameendelea kuibuka wakihoji kwanini mechi hiyo isifanyike baada ya mkutano huo kwani kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya kimataifa, mechi huweza kuangukia ndani ya siku tatu tofauti.
Ramadhan Hamis na Juma Mnonji ambao ni wanachama wa klabu ya Simba, walisema serikari inapaswa kuingilia kati kwa kushauri  zaidi ili kuweka mambo sawa katika kukwepa mwingiliano huo kutokana na umuhimu wa mkutano mkuu na mechi hiyo dhidi ya Uganda itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa.
“Tunadhani si busara mambo haya mawili muhimu kufanyika siku moja, kwani mechi ingeweza kuangukia siku yoyote kati ya tatu kwa mujibu wa kanuni za michuano ya kimataifa, hivyo kutoa nafasi ya kutosha kwa wahusika kujikita zaidi kwenye mkutano na mechi hiyo,” alisema Mnonji akiungwa mkono na Hamis.
Mnonji amekwenda mbali na kumsihi Rais wa TFF, Leodegar Chilla Tenga  kusikia malalamiko hayo ili kuondoa kiwingu kilichopo kwani hawaoni haja ya siku hiyo moja kuwa na matukio hayo mawili makubwa, kwamba mechi inaweza kuchezwa Julai 14.
Wadau wa soka wamekuwa wakiusubiri kwa hamu mkutano mkuu kutokana na umuhimu wake juu ya mustakabali wa uchaguzi mkuu ambao ulikuwa ufanyike Februari 24, lakini ukiota mbawa baada ya kuibuka mvutano.

Kwa mazingira hayo, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeagiza kuundwa kwa Kamati ya Maadili itakayohusika moja kwa moja, itakayokuwa ikifanya maamuzi ya kimaadili kwa mujibu wa kanuni za shirikisho hilo.