USHIRIKI WA SIMBA NA YANGA KAGAME:TFF YASUBIRI HURUMA YA SERIKALI

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema linasubiri tamko rasmi la Serikali juu ya ushiriki wa timu za Simba na Yanga katika michuano ya klabu bingwa Afrka Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’ iliyopangwa kufanyika Juni 18 hadi Julai 2 nchini Sudan.
Hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa machafuko katika jimbo la Darfur nchini humo ambako tayari baadhi ya timu zimetangaza kutoshiri mashindano hayo kwa hofu ya hali ya kiusalama.
Kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa  Benard Membe alisema hivi karibuni kwamba haoni kama kuna umuhimu wa Tanzania kushiriki katika michuano hiyo.
Rais wa TFFLeodger Tenga amesema leo  kwamba tayari wameshakutana na viongozi wa serikali yaani Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo pamoja na Wizara ya Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ajili ya kuzungumzia suala hivyo.
Alisema katika kikao baina ya Tff na Serikali waliwasilisha taarifa za hali halisi ya usalama ulivyo nchini Sudan pamoja na uhakika wa timu kushiriki mashindano hayo hivyo kilichobaki ni serikali kujiridhisha kwa kuhakikisha kama hali ni shwari ama la na kutoa tamko lake.
“Serikali ndiyo yenye mamlaka ya mwisho juu ya ushiriki wetu kwenye Kombe la Kagame na tunachukulia uzito kauli ya Waziri ndiyo maana tumekuwa katika majadiliano,tunasubiri maamuzi ya serikali kwani hili sio suala la TFF na hakuna mvutano katika hili na tunatumaini serikali itatoa ruhusa,”alisema Tenga.
Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) aliongeza kwamba awali mashindano hayo yalikuwa yafanyike nchini Ethiopia kabla ya kusema hawako tayari kuyaandaa na ndipo Sudan ikaamua kubeba jukumu hilo.
“Kabla ya kuwakubalia suala la machafuko lilikuja mezani lakini walituhakikishia hali ni shwari na pia masuala ya malazi, usafiri n.k yapo sawa, hivyo Cecafa tukamtuma katibu wetu huko na alipokwenda kufanya ukaguzi aliliridhika na yale tuliyoambiwa hivyo tukapisha,”alisema
Aidha, Tenga aliishukuru Sudan kukubali na kujitolea kuwa wenyeji wa michuano hiyo kutokana na ukweli kwamba ni vigumu kuyaendesha masahindano haya, pia maendeleo ya soka hayaji hivihivi.
Hata hivyo, Tenga alisema hana taarifa ya kujitoa kwenye michuano hiyo zikiwemo timu mwenyeji El Merreikh na Al Hillal na kusema kuwa atalifanyia kazi,huku kuhusiana na Tusker ya Kenya kujitoa kwenye michuano hiyo akisema huwezi kumlazimisha mtu kucheza.


Comments