STARS KAMBINI TENA JULAI KUJIANDAA NA CHAN

Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameiita tena kambini timu hiyo Julai 4 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini. 
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inavunja kambi leo (Juni 17 mwaka huu) baada ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, kundi C Kanda ya Africa dhidi ya Ivory Coast iliyochezwa jana (Juni 16 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Kim amesema wachezaji watakaoitwa kambin ni wote walioko kwenye timu hivi sasa isipokuwa Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza mpira nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) katika klabu ya TP Mazembe Englebert. 
Wachezaji hao ni Juma Kaseja, Aishi Manula, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi. 
Mechi hiyo namba 37 dhidi ya Uganda (The Cranes) itachezwa jijini Dar es Salaa kati ya Julai 12 na 14 mwaka huu wakati ile ya marudiano itafanyika wiki mbili baadaye katika Uwanja wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala.