SERIKALI:RUKSA SIMBA NA YANGA KUSHIRIKI KAGAME

SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeziruhusu timu za Simba, Yanga pamoja na Falcon ya Visiwani Pemba kushiriki michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame ambayo imepangwa kufanyika kuanzia Juni 18 nchini Sudan.
Ruhusa hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Amos Makala ambaye alisema wamelazimika kutoa ruhusa hiyo baada ya kupata barua ya uthibitisho wa kuwepo kwa Ulinzi wa kutosha kwa timu za Tanzania kutoka kwa Waziri wa Michezo wa huko.
Awali Serikali ilizuia timu hizo kwenda nchini humo kutokana na kuwepo kwa machafuko katika jimbo la Darfur.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliendelea kufanya mazungumzo na Serikali huku likiwasilisha vielelezo vya kuwepo kwa uhakika wa usalama.
Kwa mantiki hiyo hiyo sasa Yanga ambayo ni mabingwa watetezi pamoja na Simba, Falcon wataungana na timu za Al Hilal, El Merreikh, Al Ahly Shandy, Elman, URA , Ports ya Djibout, Rayon ya Rwanda na Vital'o ya Burundi katika michuano hiyo.