SERIKALI YAPIGILIA NYUNDO YA MWISHO KOMBE LA KAGAME

WAKATI Serikali ikibariki rasmi kuwa timu za Simba, Yanga na Falcon ya Zanzibar, hazitashiriki michuano inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema haliwezi kupingana uamuzi huo.
Jana bungeni mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla (pichani), alitoa kauli rasmi ya serikali, wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Sumve, Richard Ndassa.
Ndassa katika swali lake, alitaka kujua msimamo wa serikali kama timu za Tanzania zitashiriki michuano hiyo ambayo iko shakani, kutokana na baadhi ya mataifa kuanza kujitoa kutokana na hali duni ya usalama nchini Sudan.
Akijibu swali hilo, Makalla alisema, ni kweli kumekuwa na taarifa za kutokuwa na usalama nchini Sudan na kwamba, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe alishalitolea ufafanuzi.
“Sisi ndani ya serikali tuna taarifa za kutosha kuwa Sudan Kusini hakuna usalama na nchi nyingine zimeendelea kujitoa, hivyo msimamo wetu kama serikali, hatuwezi kupeleka timu sehemu isiyo na usalama,” alisema Makalla.
Juni mosi mwaka huu, Waziri Membe wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya wizara yake, alisema kwamba, anashangaa kuona Sudan ikipewa uenyeji wa michuano hiyo licha ya kuwa na usalama mdogo.
Alisema kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kwenye nchi zenye machafuko ili michuano kama hiyo iweze kufanyika ni lazima sehemu husika wanakofikia wachezaji na maofisa wengine kuwe na magari maalumu ya kuzuia risasi (bullet proof) ya kuwabeba kutoka uwanja wa ndege hadi sehemu wanakokwenda.
Waziri Membe, alihoji busara iliyotumiwa na Cecafa kuteua nchi hiyo kuwa mwenyeji wa michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 18.
Akizungumzia hali hiyo jana, Katibu Mkuu wa TFF Angetile Osiah, alisema, Serikali ndiyo yenye mamlaka ya mwisho juu ya suala hilo na kama imeona hali hairuhusu kwa Simba na Yanga kwenda huko, hawana budi kuheshimu uamuzi hao.
“Haya mashindano yapo chini ya Cecafa, hivyo hatuwezi kuyazungumzia zaidi, lakini kama wasimamizi wa soka nchini hatuna budi kufuata maelekezo ya Serikali, kwani ndiyo ina uamuzi wa mwisho,” alisema
Mwalusako aliongeza kwamba, timu yake imekuwa katika maandalizi si kwa ajili tu ya ushiriki wa michuano hiyo, kwani kuna ligi kuu, klabu bingwa ya Afrika na hata mechi kadhaa za kirafiki.
Naye Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ alisema, wakipata rasmi taarifa ya Serikali, uongozi utakutana na kuamua nini cha kufanya.